Burkina Faso inakabiliwa na hali ya dharura ambayo haikutarajiwa- WFP

16 Agosti 2019

Burkina Faso inakabiliwa na hali ya dharura ya kibinadamu kufuatia ongezeko la ukosefu wa usalama katika maeneo mengi ya ukanda wa Sahel.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi msemaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, Herve Verhoosel amesema hali hiyo inatia wasiwasi kuhusu uhakika wa chakula kwa takriban watu 688,000 hususan wakati wa msimu wa kiangazi kati ya Jmiezi ya uni na Septemba wakati hifadhi ya chakula ni ndogo ikisubiria msimu wa mavuno.

Bwana Verhoosel amesema watu kufurushwa makwao kumeongezeka mara tano zaidi tangu mwezi Desemba mwaka 2018 na hadi sasa watu takriban 240,000 wamekimbia makwao kwa mujibu wa takwimu rasmi.

Aidha ukosefu wa usalama umesababisha kufungwa kwa vituo vya afya na shule na kuathiri takriban watoto 330,000.

WFP kwa sasa inatoa msaada wa chakula kwa watu ambao wameathiriwa na dharura ya sasa pamoja na jamii ambao wanakabailiwa na ugumu wa kupata mlo wakati huu wa kiangazi.

Tangu mwezi Januari mwaka huu hadi sasa WFP imesaidia zaidi ya wakimbizi wa ndani 100,000.

Bwana Verhoosel amesema kwa ujumla WFP, inatarajia kufikisha msaada kwa watu 700,000 nchini Burkina Faso ikiwemo wakimbizi wa ndani, wanaohifadhiwa na jamii jirani na jamii zinazowahifadhi.

WFP inaendelea kutoa msaada wa lishe kwa ajili ya kuzuia na kutibu utapiamlo miongoni mwa wakimbizi wa ndani na watu walioathirika kutokana na msimu huu hususan watoto walio katika ya miezi 6 hadi miaka 5 na wanawake waja wazito na wale wanaonyonyesha.

Kwa kuzingatia hali ya sasa, WFP imesisitiza kwamba hatua madhubuti zinahitajika ili kukabiliana na hali ya sasa lakini muhimu zaidi ni kukabiliana na kiini cha mzozo wa Sahel ikiwemo umasikini, mabadiliko ya tabianchi na ujumuishwaji wa jamii.

WFP imetaka jamii ya kimataifa kuunga mkono shirika hilo katika kuhakikisha uwasilishaji wa misaada kwa Burkina Faso na ukanda wa Sahel.

Kwa sasa shirika hilo linahitaji dola milioni 35.3 kugharamia mahitaji ya sasa kufikia mwisho wa mwaka huu nchini Burkina Faso.

Taarifa hii imetolewa baada ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, David Beasley kukamilisha ziara yake ya siku mbili nchini Burkina Faso tarehe 14 mwezi huu wa Agosti ambako alikutana na rais Roch Marc Kabore, Waziri Mkuu na baadhi ya mawaziri na kuwahakikishia msaada wa WFP kwa watu wanaokabiliwa na changamoto hususan kaskazini mwa nchi hiyo.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud