Mkuu wa WFP ziarani Ghouta Mashariki nchini Syria

23 Oktoba 2018

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakla duniani, David Beasley yuko ziarani nchini Syria ambapo anatembelea maeneo ya Ghouta Mashariki na viunga vya mji mkuu Damascus, maeneo ambayo awali yalikuwa yamezingirwa na vikundi vilivyojihami na hivyo kukwamisha harakati za mashirika ya binadamu kufikisha misaada.

Akiwa huko Ghouta Mashariki, Bwana Beasley ametembelea kituo cha mgao wa chakula kwa wanafunzi shuleni pamoja na wakazi wa eneo la Zamalka wanaopata mgao wa chakula kutoka WFP.

Akizungumzia ziara hiyo,  msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi Herve Verhoosel amesema kuwepo kwa utulivu katika maeneo mengi ya Syria kumetoa fursa kwa familia kurejea katika makazi yao hata hivyo, “wengi wao wamebaini kuwa makazi yaoe  yameharibiwa na mbinu zao za kujipatia kipato hazipo tena.”

“Takribani wakimbizi wa  ndani 963,000 wamerejea kwenye makazi yao mwaka huu ikiwa ni sawa na asilimia 58 ya waliorejea kwenye makazi yao ya awali mwaka jana. Wakimbizi 23,400 pia wamerejea Syria ku toka nchi jirani za kiarabu,” amesema Bwana Verhoosel akisema kwamba kuimarika kwa usalama, utulivu na kufunguliwa upya kwa njia za kusambaza misaada na bidhaa kumesaidia pia kushuka kwa bei za vyakula.

Bwana  Verhoosel amesema kwa wastani tangu mwezi disemba mwaka 2016 ambapo bei za vyakula zilipanda kupita kiasi, hivi sasa hali ni shwari na kwa wastani bei ya kikapu kimoja cha mlo kimeshuka kwa asilimia 40.

Pamoja na idadi ya wasyria wanaorejea  nyumbani kuongezeka, WFP ina hofu na ongezeko la ukosefu wa ajira likisema linatahija doka milioni 136 hadi mwezi Machi mwakani ili kuweza kukidhi mahitaji ya wanaorejea ikiwemo mlo wa shuleni na kukwamua kipato cha familia.

Kesho Bwana Beasley atatembelea Lebanon ambako atakuana na Waziri Mkuu na pia atatembelea miradi ya WFP katika nchi hiyo ambayo inahifadhi wakimbizi milioni moja kutoka Syria ambapo 700,000 kati yao wanapokea misaada ya WFP.

TAGS: WFP, David Beasley, Syria,

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud