Miaka 70 ya mkataba wa kimataifa wa Geneva, Baraza la Usalama lajadili mbinu za kuimarisha sheria za kibinadamu

13 Agosti 2019

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumanne limekutana kujadili mbinu za kuimarisha sheria za kibinadamu za kimataifa katika mizozo ya zama hizi wakati huu wa kuadhimisha miaka 70 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa Geneva.

Akihutubia kikao hicho, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kisheria na kitengo cha Umoja huo sheria, Miguel de Serpa Soares amesema, “kujumuishwa kwa ibara jumuishi ya 3 katika mkataba wa kimataifa wa Geneva ulikuwa ni wakati wa kihistoria kwa utu,  kwani ilikuwa ni mara ya kwanza ambapo mizozo ya vikundi vilivyojihami visivyo vya kimataifa vilikuwa chini ya makubaliano ya mataifa.”

Bwana De Serpa Soares ameongeza kwamba, “hakuna mjadala kwamba ibara ya  3 ni moja ya viungo muhimu vya mkataba wa kimataifa wa Geneva, kwani labda ni moja ya makubaliano yanayotumika katika mizozo ya makundi yaliyojihami ambayo mara nyingi hayana sura ya kimataifa.”

Kwa upande wake Rais wa shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu duniani, ICRC Peter Maurer akihutubia baraza hilo kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi amesema, mkataba huo wa Geneva, “unaashiria sehemu ya pamoja ya utu wetu, na inatukinga kutokana na unnyama wetu.”

Bwana Maurer ameongeza kwamba, “maadhimisho haya yanatoa changamoto kwamba kuzingatia sheria kunawezekana na kunapendeza kwetu sote. Pia ni wito wa kufanya mengi zaidi, kufanya kwa ubora zaidi na kuishi kufikia wajibu wetu wakati wa mzozo na kulinda Maisha na hadhi.”

Naye Annyssa BelIal kutoka Chuo cha Geneva cha sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu ameliambia baraza hilo kwamba, “kuyataja makundi yaliyojihami kama kundi la kigaidi kunakwamisha uwezekano wa ushirikiano kwa misingi ya kibinadamu kwa makundi hayo.”

BelIal ameongeza kwamba, “wataalam wanakubaliana kwamba ni muhimu kuwaza makundi ya watu waliyojihami kama wakiukaji wa haki za kimataifa za kisheria, lakini pia kama watu muhimu katika utekelezaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, kwa sababu mara nyingi wanakuwa karibu na watu wanaowakilisha.”

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland Jacek Czaputowicz ambao ndio wanashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Agosti, amesema, “majadiliano ya leo yameibua ukweli kwamba sheri za za kimataifa za kibinadamu hazizingatiwi hususan katika maeneo kama Syria, Libya, Sudan Kusini au Ukraine.”

Mkataba wa kimataifa wa Geneva ulipitishwa tarehe 12 mwezi Agosti mwaka 1949 kwa ajili ya kulinda makundi yaliyo hatarini kwenye mizozo baina ya makundi yaliyojihami.

Makundi hayo  yaliyo hatarini ni pamoja na majeruhi, wagonjwa, wafungwa wa vita, raia wakiwemo wale wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter