Hatua kali ni lazima katika kuzuia kuenea silaha za maangamizi-SC

26 Septemba 2018

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametaka mshikamano na hatua kali kutoka kwa baraza hilo dhidi ya silaha za maangamizi zikiwemo za nyuklia, kibaolojia na za kemikali.

Wajumbe wametoa wito huo hii leo katika kikao cha ngazi ya mawaziri cha wajumbe wote 15 kilichoitishwa na Marekani kandoni mwa mjadala wa baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kujadili njia za kulifanya Baraza hilo ambalo lina dhamana ya kusimamia amani na usalama wa kimataifa kuweza kuhimiza utekelezaji wa maazimio yanayopinga kuenea kwa silaha za maangamizi (WMD) kama vile nyuklia, silaha za kibaolojia na za kemikali.

Mwenyekiti wa kikao hicho Rais Donald Trump  wa Marekani akifungua mjadala huo amesema hatua kali zichukuliwe dhidi ya mataifa ambayo yanakiuka maazimio ya Baraza la Usalama kuhusu uenezaji na matumizi ya silaha hizo.

Akitolea mfano Iran amesema “Katika miezi ijayo Marekani itaiwekea vikwazo vigumu zaidi kuliko hapo awali miezi kufuatia kujitoa kwake mapema mwaka huu kwenye makubaliano ya kimataifa ya kudhibiti mipango ya nyuklia ya taifa hilo” yanayojulikana kama mpango madhubuti wa kuchukua hatua (JCPOA) yaliyofikiwa baina ya Iran, China, Ufaransa, Ujeriumani , Urusi, na Uingereza. Na kisha akatoa wito

(SAUTI YA DONALD TRUMP)

“Nawaomba wajumbe wote wa baraza la Usalama kushirikiana na Marekani kuhakikisha utawala wa Iran unabadili mwelekeo wake , na kuhakikisha asilani haitomiliki bomu la nyuklia.”

Kwa upande wa tishio dhidi ya maisha ya mamilioni ya watu linaloendelea Syria Trump ameishukuru Iran, Urusi na Syria kwa kupunguza mashambulizi mjini Idlib japo amesisitiza kuwa matumizi ya silaha zozote za maangamizi hayatovumiliwa.

Wajumbe wengine wote waliozungumza wamesisitiza umuhimu wa kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa kuheshimu maazimio ya Baraza la Usalama kwa maslahi ya wengi na kuwa msitari wa mbele kufanikisha na sio kukwamisha azma hiyo. Teressa May ni waziri mkuu wa Uingereza

Teressa May ni waziri mkuu wa Uingereza akihutubia Baraza la Usalama Septemba 26 2018
UN Photo/Evan Schneider
Teressa May ni waziri mkuu wa Uingereza akihutubia Baraza la Usalama Septemba 26 2018

 

(SAUTI YA TERESSA MAY)

“Tunahitaji kuona maamuzi zaidi ya pamoja katika Baraza hili kukabiliana na usafirishaji na uenezaji wa teknolojia za silaha hizi na kuongeza gharama kwa wahusika , ni jambo la kusikitisha kwamba Urusi inaendelea kuzuia Baraza kutekeleza majukumu yake ya kuzuia shughuli hizi  zenye maafa.”

Wajumbe wote wameafiki kuwa kupinga kuenea kwa silaha za maangamizi sio chaguo ni lazima , akifafanua hilo katika mkutano waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Dkt. Workneh Gebeyehu amesema

 

“Kwa hakika kuenea silaha za maangamizi kunatoa tisho kubwa kwa Amani na usalama wa kimataifa kuanzia DPRK , masuala ya nyuklia ya Iran, hadi mashambulizi ya kemikali huko Syria na tukio la Salisbury Uingereza".

Hatari ya kuenea kwa silha hizo imekuwa moja ya changamoto kubwa kabisa ya wakati wetu, na mpango wa kimataifa wa kuzuia kuenea kwa silaha hizo uko katika changamoto kubwa na hofu ya kuenea kwa silaha hizo iki katika kiwango cha juu kabisa tangu vita ya pili ya dunia.

Kama alivyosema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  tunaamini kwamba ni muhimu sana kwa pamoja kushughulikia hatari za kuenea kwa silaha hizi sio kama chaguo bali kujaribu kusaka suluhu ya baadhi ya masuala magumu yanayotukabili hivi sasa kwa njia za kisiasa na kidiplomasia.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter