Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yabisha hodi Lodja, jimboni Kasai-Mashariki kuepusha majanga zaidi

MONUSCO yashiriki kurejesha amani huko Lodja, DRC
MONUSCO
MONUSCO yashiriki kurejesha amani huko Lodja, DRC

MONUSCO yabisha hodi Lodja, jimboni Kasai-Mashariki kuepusha majanga zaidi

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri  ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO,  umechukua hatua kuzuia majanga zaidi kwenye eneo la Lodja lililopo jimbo la Kasai Mashariki.

Eneo hilo limekuwa na ghasia za mara kwa mara nagu uchaguzi wa gavana wa Sankuru tarehe 20 mwezi uliopita wa Julai, ghasia zilizoambatana na mauaji na uharibifu wa nyumba.

Ni kwa kuzingatia hali hiyo, MONUSCO tangu tarehe mosi hadi 6 ya mwezi huu wa Agosti ilipeleka timu yake kusaidia kurejesha amani.

Firmin Koné, ambaye ndiye aliongoza ujumbe huo wa MONUSCO amesema lengo lao ni kuweka mazingira muhimu ya mfumo wa mashauriano unaoweza kutumika hata siku za usoni pindi kuna mzozo.

Wakiwa kwenye eneo hilo, ujumbe huo wa MONUSCO ulibaini nyumba 142 zilizochomwa moto na watu kwenye kitongoji cha Nambelo na watu ambao kwa mujibu wa mashuhuda walitoka Kondo-Shumbe, ikidaiwa kuwa walichukua hatua hiyo kufuatia kifo cha chifu wao wa kijadi.

Wakati wa ziara yao, ujumbe huo wa MONUSCO uliendesha mafunzo ya kusaka suluhu ya mzozo kwa amani pamoja na kuwa na mikutano kadhaa na viongozi wa kijamii kutoka Kondo Shumbe, Hiyanja na Kambeguete, pamoja na wajumbe wa baraza la eneo la Lodja, mashirika ya kiraia na wawakilishi wa jamii za misitu za huko Tetela na Savanna.

MONUSCO inasema kuwa viongozi wa kidini nao pia walialikwa.

Jumla ya mapendekezo 28 yalipitishwa na washiriki wa mkutano huo wa kujenga amani huko Lodja.