Kuahirishwa kwa uchaguzi DRC kuimarishe mazingira ya upigaji kura- Baraza

22 Disemba 2018

Wajumbe wa Baraza laUsalama la Umoja wa Mataifa wamesema wametambua uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, CENI ya kuahirisha hadi tarehe 30 mwezi huu uchaguzi wa rais, wabunge na majimbo ambao ulikuwa ufanyike kesho Jumapili.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo mjini New York, Marekani, wajumbe hao pamoja na kutambua hatua hiyo ya CENI, pia wamesisitiza azma yao ya dhati ya kuzingatia mamlaka, uhuru na umoja wa taifa hilo.

Hata hivyo wajumbe hao wameelezea matumaini ya kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi huo kutatoa fursa ya maandalizi bora kwa wananchi wa DRC kutekeleza haki yao hiyo kwa uhuru tarehe 30 mwezi huu wa Desemba.

Wametaka muendelezo wa mjadala na uwazi baina ya wadau wote wakati wa kipindi hiki ili kuhakikisha  uchaguzi wa amani na wenye uwazi ambao utawezesha kubadilika kwa serikali kwa mujibu wa katiba ya DRC pamoja na makubaliano ya tarehe 31 mwezi Desemba mwaka 2016.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametumia taarifa yao pia kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliofariki dunia kwenye ajali ya ndege iliyokuwa imekodishwa na CENI kwa ajili ya shughuli za maandalizi ya uchaguzi.

Vile vile wameunga mkono juhudi   za tume hiyo za kuhakikisha kuwa vifaa vinavyohitajika  vinafika kwa wakati popote vinakohitajika kabla ya siku ya uchaguzi ambapo wamekariri utayari ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wa kutoa msaada wakati wowote utakapohitajika.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter