Kuwait yaunga mkono juhudi za kupunguza njaa nchini Syria

7 Agosti 2019

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, hii leo mjini Cairo Misri na Roma Italia limekaribisha na kushukuru mchango wa dola milioni tatu kutoka Kuwait ili kuwasaidia watu 20,000 walioko katika hali ya hatari pamoja na ndugu zao nchini Syria.

Mwakilishi wa kudumu wa serikali ya Kuwait katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva Jamal Al-Ghunaim amesema, “serikali ya Kuwait inajitolea kusaidia watu walio na uhitaji wa msaada wa kibinadamu. Ni muhimu kurejesha na kuimarisha ustawi wa kilimo na uhakika wa chakula wa watu wa Syria.”

Naye Mkurugenzi Mkuu msaidizi na mwakilishi wa FAO kanda ya mashariki ya kati na Afrika kaskazini (NENA) Bwana Abdessalam Ould Ahmed amesema, “mchango huu wa ukarimu utaenda mbali sana na umekuja wakati muafaka. Utaisaidia FAO kuendeleza juhudi zake za kusaidia uhakika wa chakula kwa jamii za wasyria na kufanya shughuli zinazolenga kuzifanya jamii zinazolima kuwa na mnepo katika kuboresha uhakika wao wa chakula na lishe.”

Kwa upana zaidi, Kuwait na FAO wanashirikiana zaidi katika kupambana na njaa na utapiamlo na kuja na msaada kwa jamii zilizotikiswa na majanga katika eneo la NENA na zaidi katika nchi kama vile Yemen, Somalia, Sudan Kusini na Nigeria.

FAO itasambaza msaada huu kutoka Syria kwa wakulima na wafugaji wapatao 20,000 waliko hatarini ili hususani familia zinazoongozwa na wanawake kuwasaidia wao jamaa zao katika masuala kama mbegu, vifaa vya umwagiliaji, vyakula vya mifugo yao na pia mafunzo ya kilimo bora. Mambo hayo yatafanyika katika maeneo ya Daraa, As-Sweida, Deir-Ez-Zor na Hama.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud