Heko AU kwa kuwa na mkutano kila mwaka kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo- Bi. Patten

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umefanya warsha maalum kwa ajili ya kusaidia wanawake ambao wamekabiliwa na ukatili wa kingono na kusihi jamii kuripoti visa hivyo ili wahalifu wawajibishwe
UNifeed Video
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umefanya warsha maalum kwa ajili ya kusaidia wanawake ambao wamekabiliwa na ukatili wa kingono na kusihi jamii kuripoti visa hivyo ili wahalifu wawajibishwe

Heko AU kwa kuwa na mkutano kila mwaka kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo- Bi. Patten

Amani na Usalama

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya  ukatili wa kingono katika maeneo yenye mizozo, Pramila Patten amepongeza uamuzi wa hivi karibuni wa Muungano wa Afrika, AU, wa kutenga mkutano mmoja kila mwaka kujadili kwa uwazi janga la ukatili wa kingono katika mizozo barani humo.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York, Marekani, Bi. Patten amesema “ajenda hii mpya iliyoanzishwa itatoa fursa ya jukwaa la kila mwaka kwa nchi wanachama wa AU na wadau wao kutathmini mafanikio yaliyopatikana na vikwazo vya kuzuia na kuadhibu uhalifu huo wa kutisha.”

Amesema kwa kutoa fursa ya kimkakati ya kupazia sauti hatua nzuri za kuepusha ukatili wa kingono vitani, halikadhalika kubadilishana mawazo na uzoefu, mkutano huo wa kila mwaka utachagiza hatua za kutokomeza vitendo hivyo ambavyo ni tishio kwa amani, usalama na maendeleo.

“Kwa kuweka suala hili kwenye ajenda ya kudumu ni kiashiria cha utashi wa kisiasa wa kubadili tamaduni za ukimya na ukwepaji sheria na badala yake kuwa na utamaduni wa uwajibikaji. Ni kiashiria pia cha azma ya kutekeleza ahadi ya kuwapatia kipaumbele manusura ikiwemo kupatiwa huduma kwa urahisi na kwa usalama na kushughulikia chanzo cha ukatili wa kingono ikiwemo mifumo ya ukosefu wa usawa wa kijinsia,” amesema Bi. Patten.

Uamuzi huo wa AU unafuatia ziara ya mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu mjini Addis Ababa, Ethiopia ambako ni makao makuu ya Muungano wa Afrika tarehe 23 mwezi uliopita wa Julai.

Wakati wa ziara hiyo Bi. Patten alihutubia kikao cha Baraza la Amani na Usalama la AU kilichokuwa na mjadala wa wazi kuhusu ukatili wa kingono kwenye maeneo ya mizozo barani Afrika.