Ili kukomesha ukatili wa ngono katika mizozo juhudi zaidi zaihitajika:EU/UN

19 Juni 2019

Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kwa pamoja wamepaza sauti wakitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi ili kukomesha mifumo yote ukatili wa kingono ikiwemo kutumika kama mkakati na mbinu za vita na ugaidi.

Kupitia ujumbe wao maalum kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kingono katika migogoro Federica Mogherini mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Ulaya (EU) kwa ajili ya sera za mambo ya nje na Pramila Patten mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uaktili wa kingono katika mizozo wamesema “ukatili wa kingono katika mizozo ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulio na athari mbaya za kimwili, kisaikolojia na kijamii, zinazoathiri maendeleo ya kiuchumi , mshikamano wa kijamii na amani na usalama wa kudumu.”

Pia wameongeza kuwa ingawa wanawake na wasichana ndio waathirika wakubwa wa jinamizi hili lakini pia wanaume na wavulana wameathirika.

Pramila Patten, Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo akifungua kikao cha Baraza la Usalama kuhusu wanawake, amani na ulinzi wa amani.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Pramila Patten, Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika mizozo akifungua kikao cha Baraza la Usalama kuhusu wanawake, amani na ulinzi wa amani.

Mogherini na Patten wamesisitiza kwamba “Ukatili wa kingono ni uhalifu ambao unazuilika na unaoweza kuepukika. Hii ndio maana Umoja wa Mataifa na Muungano wa Ulaya wamejizatiti kuimarisha kazi zao katika kuziia, kulinda na kuwachukulia hatua wahusika, pamoja na kutoa msaada kwa waathirika ili waweze kujenga upya maisha yao katika familia zao na jamii zao .”

Kwa pamoja EU na UN wameshirikiana katika miradi mbalimbali kwa mfano mradi unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambao uliosaidia kuanzishwa kwa mfumo wa kuendesha mashitaka utakaowasaidia viongozi wa kijeshi kuwafikisha wahusika wa makosa makubwa ikiwemo ukatili wa kingono mbele ya sheria.

Mafanikio

Mradi huu umesaidia kuwabaini na kuwawajibisha wahalifu wote wa jeshi la serikali na makundi yenye silaha ambao la sivyo wangeendelea kukwepa sheria.

Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Ulaya Federica Mogherini akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa ushirikiano baina ya UN na EU 2019
UN Photo/Manuel Elías
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Ulaya Federica Mogherini akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano wa ushirikiano baina ya UN na EU 2019

Viongozi hao wamesema hatimaye hatua za mashirika yao hatiumaye zimaweza kuleta mabadiliko ya kudumu zikiunganishwa na kubadilika kwa mtazamo wa jamii ambao unaweza kufikiwa na kuelimishwa kwa kupaza sauti za waathirika na kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi na mchakato wa amani.

Wamekumbusha kwamba nchi, mashirika yakimataifa na kikanda, sekta binafsi na asasi za kiraia wote wana jukumu la kufanya katika kupinga hukka mbaya za ukandamizaji wa masuala ya kijinsia na kuzia ukatili wa kingono.

Patten na Mogherini wamesema”Leo hii tunaahidi kuendelea kufanya kazi pamoja kukomesha ukwepaji sheria kwa wahusika wa ukatili wa kingono katika mizozo na kuhakikisha fursa ya waathirika kupata haki, ulinzi na huduma.Sauti zao, haki zao na mahitaji yao yanapaswa kuwa muongozo wa hatua zetu wa kuhakikisha jamii zinazojiweza na za amani.”

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter