Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili na unyanyasaji wa kingono marufuku UN: Ripoti

Picha: UM/Evan Schneider (Maktaba)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (wa pili kutoka kulia) akihutubia mkutano wa ngazi ya juu kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono.

Ukatili na unyanyasaji wa kingono marufuku UN: Ripoti

Wanawake

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatua za ulinzi dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kingono (SEA) imetolewa leo ikiainisha hatua zilizochukuliwa na nani waliohusika katika juhudi kukomesha hali hiyo. 

Ripoti hiyo ya mtazamo mpya unaochukuliwa na Umoja wa Mataifa kukomesha uhalifu huo imejumuisha taarifa za madai ya ukatili huo unaodaiwa kufanywa na operesheni za ulinzi wa amani na operesheni zingine za kisiasa , mashirika ya Umoja wa mataifa na vikosi vya kimataifa visivyo vya Umoja wa Mataifa ambavyo vimeruhusiwa kulinda amani na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Inajumuisha matukio ya kuanzia Januari Mosi hadi Desemba 31 mwaka 2017. Ripoti inasema kumekuwa na jumla ya madai 138 ya ukatili na unyanyasaji wa kingono 2017, madai 62 ni dhidi ya operesheni 10 za ulinzi wa amani na moja ya operesheni za masuala ya kisiasa, huku madai 41 yakihusisha wanajeshi 101, Madai 10 yakihusisha polisi 23 na Madai 11 yakuhusisha wafanyakazi wa kiraia wa Umoja wa Mataifa.

Pia Madai 75 kati ya 138 yanahusisha mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa ambayo ni la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la uhamiaji IOM, la kuhudumia watoto UNICEF, la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, la idadi ya watu UNFPA , la mpangomwa chakula WFP, UN Women, OCHA, UNPOS na 25 kati ya Madai hayo 75 yanahusu mashirika wadau wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba ukatili huo hauwezi kuvumiliwa na hatua madhubuti zinaendelea kuchukuliwa ikiwemo sheria kushika mkondo wake kwa watakaothibitishwa kuhusika . Visa vingi bado vinaendelea kuchunguzwa.