Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jeshi la Myanmar lastahili vikwazo vikiwemo vya silaha:Tume ya UN

Wakimbizi waRohingya wanaokimbia mzozo na manyanyaso nchini Myanmar.
IOM/Mohammed
Wakimbizi waRohingya wanaokimbia mzozo na manyanyaso nchini Myanmar.

Jeshi la Myanmar lastahili vikwazo vikiwemo vya silaha:Tume ya UN

Haki za binadamu

Tume huru ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa nchini Myanmar imeitaka jumuiya ya kimataifa kukata uhusiano na jeshi la Myanmar na mtandao mkubwa wa makampuni linayoyathibiti na kuyategemea na kuliwekea vikwazio vikiemo vya silaha.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na tume hiyo ya kimataifa inasema mapato yanayokusanywa na jeshi hilo kutokana na mikatab ya biashara ya ndani na ya nje yameimarisha uwezo wa jeshi hilo kuendelea kutekeleza ukiuykwaji mkubwa wa haki za binadamu na kukwepa sheria.

Ripoti ya uchunguzi wa tume hiyo kwa mara ya kwanza imeainisha kwa kina kiwango ambacho jeshi la Myanmar linatumia biashara zake, makampuni ya nje na mikataba ya biashara ya silaha kusaidia operesheni zake dhidi ya makundi ya kikabila kitu ambacho ni uhalifu mkubwa chini ya sheria za kimataifa kutojali raia na kukwepa uwajibikaji.

Tume hiyo ya uchunguzi imesema”Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi wanachama viyawekee vikwazo mara moja makampuni yanayoendeshwa na jeshi la nchi hiyo linalojulikana kama Tatmadaw.” Pia imewachagiza wateja , wawekezaji na makampuni nyumbani Myanmar na nje ya nchi kujihusisha na biashara ambazo hazina uhusiano na jeshi.

Wakina mama wakimbizi wa kabila la warohingya wakiwa na watoto wao wakisubiri watoto wao wachunguzwe katika kituo cha tiba huko Cox's Bazar nchini Bangladesh
UNICEF/Bashir Ahmed Sujan
Wakina mama wakimbizi wa kabila la warohingya wakiwa na watoto wao wakisubiri watoto wao wachunguzwe katika kituo cha tiba huko Cox's Bazar nchini Bangladesh

Tume hiyo pia imetoa wito wa “kuweka vikwazo vya silaha , ikitaja makampuni makampuni 14 ya kigeni kutoka nchi saba ambayo yamekuwa yakiliuzia jeshi hilo ndege za kivita, magari ya kivita, meli za vita, makombora na vifaa vya kurushia makombora tangu mwaka 2016.”

Katika kipindi hicho kwa mujibu wa tume ya uchunguzi jeshi lilitekeleza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia kwenye majimbo ya Kachin, Shan na Rakhine ikiwemo kuwarejesha kwa nguvu Bangladesh watu wa kabila la Rohingya zaidi ya 700,000.

Ripoti ya tume hiyo imeyaanika hadahrani makampuni maarufu na makubwa mawili nchini Myanmar ambayo yanamilikiwa na maafisa wa ngazi za juu jeshini ambayo ni Myanmar Economic Holdings (MEHL) na Myanmar economic Corporation (MEC).

Watoto wa kabila la warohingya kutoka Myanmar wakicheza kwenye kambi ya wakimbizi ya Kutupalong nchini Bangladesh tarehe 21, Novemba 2018 na kontena za maji safi na salama zikiwa pembeni.
© UNHCR/Roger Arnold
Watoto wa kabila la warohingya kutoka Myanmar wakicheza kwenye kambi ya wakimbizi ya Kutupalong nchini Bangladesh tarehe 21, Novemba 2018 na kontena za maji safi na salama zikiwa pembeni.

Na miongoni mwa wamiliki wa makampuni hayo ni mkuu wa majeshi Jeneral Min Aung Hlaing na naibu kamanda mkuu Jeneral Soe Win ambao wote tume hiyo ahapo awali ilisema wachunguzwe na kufunguliwa mashitaka kwa mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa vita.

Tume inasema makampuni hayo mawili yanamiliki biashara zaidi ya 120 yakihusisha kila kitu kuanzia ufisadi, madawa, viwanda, bima, utalii na benki.

Na makampuni hayo pia pamoja na vitengo vyake zaidi ya 26 ndio yenye leseni za migodi ya madini ya Jade na Rubi kwenye majimbo ya Kachin na Shan.

Tume hiyo inasema ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu,ikiwemo utumikishwaji wa lazima na ukatili wa kingono umetekelezwa na Tatmadaw Kaskazini mwa Myanmar ukihusiana na shughuli zao za kibiashara.