Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo nchini Myanmar unaelekea kuwa vita kamili aonya Bachelet  

Watu wakifanya hafla ya kuwakumba waliopeteza maisha Yangon Myanmar.
Unsplash/Zinko Hein
Watu wakifanya hafla ya kuwakumba waliopeteza maisha Yangon Myanmar.

Mzozo nchini Myanmar unaelekea kuwa vita kamili aonya Bachelet  

Haki za binadamu

Ukandamizaji dhidi ya waandamanaji unaoendelea nchini Myanmar unaweza kusababisha mzozo kuwa vita kamili sawa na Syria, ameonya leo Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, akiyataka Mataifa yenye ushawishi kuchukua hatua za haraka na zenye ufanisi kukomesha mauaji ya raia nchino humo. 

“Matamko ya kulaani, na vikwazo vichache kwa walengwa maalum, havitoshi. Mataifa yenye ushawishi yanahitaji kutoa shinikizo la pamoja kwa wanajeshi nchini Myanmar ili kusitisha tume ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uwezekano wa uhalifu dhidi ya binadamu”,  amesema Kamishina mkuu huyo Michelle Bachelet. 

Wito wake umekuja baada ya kuwa na mwisho wa wiki mwingine tena ulioghubikwa na "umwagikaji wa damu uliopangwa" huko Myanmar, pamoja na mauaji yaliyoripotiwa ya watu wasiopungua 82 huko Bago, ambapo, kulingana na ripoti za kuaminika, jeshi la nchi hiyo, Tatmadaw, lilifyatua risasi na mabomu ya kurusha roketi, mabomu ya kugawanyika na vilipuzi. 

Bi Bachelet ameongeza kuwa "Wanajeshi wanaonekana kuwa na nia ya kuimarisha sera yao isiyo na huruma na ya unyanyasaji dhidi ya watu wa Myanmar, wakitumia silaha za kiwango cha kijeshi na za kibaguzi", 

Vikosi vya usalama pia vimeripotiwa kuwazuia wahudumu wa afya kuwasaidia  watu waliojeruhiwa, na vile vile kuwatoza jamaa "faini" ya takriban dola 90 kudai miili ya wale waliouawa, kwa mujibu wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa haki za binadamu (OHCHR), ambayo imeongeza kuwa watu wengine sasa wameamua kutumia silaha za kiasili au za zamani katika kujilinda. 

Bi Bachelet pia ameangazia hitaji la kukomesha usambazaji wa silaha na fedha kwa uongozi wa jeshi ambao unasaidia tume yake ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, akibainisha ripoti ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli wa juu ya Myanmar, ambayo ina mapendekezo wazi ya hatua zinazofaa kuhusiana na jeshi. 

Mwangwi dhahiri wa kama yaliyojiri Syria 

Kamishna Mkuu ameonya kuwa hali nchini Myanmar ni mwangwi wa wazi wa yake yaliyojiri Syria mnamo 2011, wakati nchi hiyo ilipotumbukia kwenye vita, na kwa miaka kumi iliyopita umedhihirisha athari mbaya kwa mamilioni ya raia. 

“Huko pia, tuliona maandamano ya amani yalikutana na nguvu isiyo ya lazima na isiyo kubalika. Ukandamizaji wa kikatili, unaoendelea wa watu wake ulisababisha watu wengine kuchukua silaha, ikifuatiwa na kuongezeka kwa kasi ya vurugu kote nchini ", amesema Bachelet. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alionya kuwa kutofaulu kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua na kufanya maamuzi ya pamoja inaweza hali kuwa mbaya kwa Syria na kwingineko, Bi Bachelet ameongeza. 

"Ninaogopa hali nchini Myanmar inaelekea kwenye mzozo kamili. Mataifa hayapaswi kuruhusu makosa mabaya ya zamani huko Syria na kwingineko kurudiwa tena. " 

Watu walilazimishwa kujificha, mtandao umekatwa 

Zaidi ya watu 700 wanaripotiwa kuuawa katika ukandamizaji na vikosi vya usalama tangu jeshi lilipoiangusha Serikali mnamo 1 Februari mwaka huu. Maelfu zaidi wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa katika hali mbaya. 

Kwa uchache watu 3,080 wako kizuizini na kuna ripoti kwamba watu 23 wamehukumiwa kifo kufuatia mashtaka ya siri wakiwemo waandamanaji wanne na wengine 19 ambao walishtakiwa kwa makosa ya kisiasa na ya jinai imesema OHCHR. 

Kukamatwa kwa watu wengi kumelazimisha mamia ya watu kujificha, na ripoti zinaonyesha kuwa waandishi wa habari wengi, wanaharakati wa asasi za kiraia, watu mashuhuri na viongozi wengine wa umma wanatafutwa, wengi kwa sababu tu ya upinzani ambao wamekuwa wakionyesha kwenye mtandao,imeongeza ofisi hiyo ya haki za binadamu. 

Huduma za runinga, mtandao na za simu za rununu pia zimekatwa kwa muda usiojulikana tarehe tangu tarehe 2 Aprili, na kuwaacha idadi kubwa ya watu bila kupata vyanzo muhimu vya habari na mawasiliano.