Mzozo Mashariki mwa Ukraine waendelea kukiuka haki za binadamu:Gilmore

10 Julai 2019

Mzozo unaoendelea Mashariki mwa Ukraine umeendelea kuwa chachu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu amesema naibu Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Kate Gilmore akiwakilisha ripoti ya robo mwaka kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Ukaine kwenye kikao cha 41 cha Baraza la Haki za binadamu kinachoendelea mjini Geneva Uswis.

Bi. Gilmore amesema katika muda ambao umefanyiwa tathimini kati ya Januari Mosi mwaka huu na Juni 30 bado visa vya mauaji na majeruhi ya raia vimeendelea kuripotiwa kwa mfano ofisi ya haki za binadamu imeorodhesha visa 91 ambavyo watu 13 wameuawa na 78 kujeruhiwa na vimechangiwa na matumizi ya silaha ndogondogo na silaha nyepesi, makombora, mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa vingine vya mlipuko na athari zake ni kwa wanawake, wanaume, wavulana na wasicha wasio na hati.

Kwa ujumla kwa mwaka huu Gilmore amesema matukio 230 ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili yameripotiwa Ukraine Mashariki yakiathiri watu 220 na ukiukwaji huo ni kuanzia haki za kimwili za utu wa mtu na kupata haki katika kesi mahakamani , hadi ukiukwaji wa haki ya kuishi, kutobaguliwa, uhuru wa msingi na haki zingine za kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kuwa ikiwa ni miaka mitano tangu kuanza kwa mzozo huko Ukraine Mashariki vita vimeendelea kuathiri watu nchi nzima hivi sasa kukiwa na watu milioni 5 ambao wameathirika moja kwa moja na vita hivyo. Na madahara yake ni hatari kwa maisha yao na kila kitu”Mwanamke mmoja mkazi wa eneo lenye mapigano amesema ni ghara kiasi gani ya utoto wa mwanangu? kutenganishwa na familia yangu kwa miaka mitatu kuna thamani kiasi gani? Kifo cha mapema cha baba yangu thamani yake ni kiasi gani? Kwa sababu hakuweza kupata msaada wa tiba aliotakiwa wakati wa vita.”

Hata hivyo ofisi hiyo ya haki za binadamu imesema ukilinganisha na wakati kama huu mwaka jana idadi ya mashambulizi imepungua kwa asilimia 52 lakini Gilmore anasema watu 91 bado ni wengi “tunaamini inawezekana kuzuia vifo na majeruhi kwa raia hata kama bado suluhu endelevu ya mgogoro bado haijapatikana. Pande husika katika vita ni lazima zichukue hatua zote za kuhakikisha zinalima Maisha ya raia na miundombinu yao.”

Bi. Gilmore amekaribisha pia uamuzi wa serikali uliochukuliwa mwezi Machi mwaka huu 2019 wa kuanzisha mkakati wa sera ya kitaifa ya kuwalinda raia katika vita na kutoa wito wa kuanzishwa mpango wa hatua kwenda sanjari na mkakakati huo.

Amesema hali ya kiuchumi inaendelea kuathiriwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine Mashariki huku watu wakiishi kwa kutengwa katika baadhi ya vijiji na kwa wale walio karibu na uwanja wa mapambano kutokana na ukosefu wa huduma muhimu.

Pia amesema sera za kibaguzi zimeendelea kugawanya watu, huku sheria na vitendo vingine kandamizi vikiendelea kuwa kikwazo cha uhuru wa watu kutembea na fursa ya kupata malipo ya uzeeni na mafao ya hifadhi ya jamii. Watu wengi wanajaribu kukimbia kutoka eneo hilo lakini wanakabiliwa na hatari kubwa kwani tangu mwanzo wa mwaka huu wa 2019 watu 30 wameuawa wakijaribu kuvuka eneo la mapambano.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter