Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN asihi kuongezwa kwa juhudi za kidiplomasia kuepusha migogoro Ukraine 

Watoto wakitembea kuelekea shuleni katika mji wa Avdiivka, Donetsk Oblast, Ukraine. (Maktaba)
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Watoto wakitembea kuelekea shuleni katika mji wa Avdiivka, Donetsk Oblast, Ukraine. (Maktaba)

Katibu Mkuu wa UN asihi kuongezwa kwa juhudi za kidiplomasia kuepusha migogoro Ukraine 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameeleza wasiwasi wake hii  leo Jumatatu kuhusu hatari ya mzozo wa kijeshi nchini Ukraine na kutoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za kidiplomasia. 

"Nina wasiwasi mkubwa na mvutano ulioongezeka na uvumi ulioongezeka wa uwezekano wa mzozo wa kijeshi huko Ulaya." Guterres amewaeleza waandishi wa habari baada ya mkutano usio rasmi wa kujadili hali ndani na karibu na Ukraine, mkutano uliofanyika jijini New York Marekani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa. 

Tangu mwezi Novemba, Urusi imekusanya zaidi ya wanajeshi 100,000 kwenye mipaka ya mashariki ya Ukraine, na hivyo kuzua wasiwasi katika nchi za Magharibi, ambazo zinahofia operesheni mpya ya kijeshi dhidi ya Ukraine, baada ya kutwaliwa kwa Crimea mwaka 2014, sambamba na mzozo uliodumu kwa muda mrefu kwa miaka minane na wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine. 

Marekani inasema Urusi inaweza kushambulia Ukraine "wakati wowote". Urusi inakanusha nia yoyote ya kichokozi kuelekea Ukraine, lakini inahusisha kupunguzwa kwa kasi na mfululizo wa madai, hasa uhakikisho kwamba haitawahi kujiunga kwenye NATO. 

Hakuna mbadala wa diplomasia 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza kwamba mzozo utakuwa janga katika suala la mateso ya binadamu, na uharibifu kwa usalama wa Ulaya na kimataifa. 

Amesisitiza kwamba ataendelea kuhusika kikamilifu "katika saa na siku zijazo" ili kuepusha migogoro na kwamba timu ya Umoja wa Mataifa nchini Ukraine inaendelea kufanya kazi kikamilifu nchini humo. 

"Hakuna mbadala wa diplomasia. Masuala yote ikiwa ni pamoja na yale yasiyoweza kutatuliwa, yanaweza na yanapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa ndani ya mifumo ya kidiplomasia. Ninaamini kwa dhati kwamba kanuni hii itashinda.” Amesema akitaka kuheshimiwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa. 

"Sasa ni wakati wa kutuliza mvutano na kutuliza matukio yanayoendelea. Hakuna nafasi ya maneno ya uchochezi. Kauli za umma zinapaswa kulenga kupunguza mivutano, na sio kuzidisha.” Amesisitiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.. 

Bwana Guterres amekaribisha wimbi la hivi karibuni la mawasiliano ya kidiplomasia na mazungumzo, ikiwa ni pamoja na mazungumzo kati ya Wakuu wa Nchi. Lakini, kulingana na yeye, bado kuna mengi ya kufanya. 

Amhiyimisha Bwana Guterres kwa kueleza namna Umoja wa Mataifa ulivyo tayari kusaoidia, "natarajia kila mtu kuongeza juhudi hizi. Nimejitolea ofisi zangu na hatutaacha juhudi zozote katika kutafuta suluhu la amani.”