Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wakimbizi wa Rohingya kambini ya Cox’s Bazar wako hatarini kwa mafuriko na maporomoko ya udongo:UNICEF

Kitengo cha kupunguZa hatari cha WFP kikikarabati maeneo yaliyoporomoka kutoka na na mvua huko Cox's Bazar
WFP/Gemma Snowdon
Kitengo cha kupunguZa hatari cha WFP kikikarabati maeneo yaliyoporomoka kutoka na na mvua huko Cox's Bazar

Watoto wakimbizi wa Rohingya kambini ya Cox’s Bazar wako hatarini kwa mafuriko na maporomoko ya udongo:UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Maelfu ya watoto na familia zinazoishi katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya mjini Cox’ Bazar kusini mashariki mwa Bangladesh wako hatarini kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa katika siku chache zilizopita, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF hii leo mjini Cox’s Bazar, Bangladesh na New York Marekani.

Taarifa hiyo ya UNICEF imeeleza pia kuwa hali mbaya hususani katika kambi ambamo zaidi ya familia 4,000 zimeathirika ingawa wengi wao tayari wamehamishiwa katika maeneo salama.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Bangladesh Alain Baland Domsam amesema, “hali katika kambi na jamii wenyeji imedorora kwa haraka kwasababu ya hali mbaya ya hewa na kuna uwezekano mahitaji ya kibinadamu hapa yakahitajika zaidi katika siku zijazo wakati ambapo mvua zaidi zinatarajiwa. Sisi pamoja na washirika wetu tumeongeza usabazaji wa mahitaji muhimu yakiwemo vidonge vya kusafishia maji na mahitaji mengine kwa watoto na familia zao.”

Kwa mujibu wa ripoti, mtoto wa kiume mmoja mwenye umri wa miaka 7 amezama na kufa maji kufuati mvua hizo kubwa na watoto wengine wawili wamejeruhiwa. Hadi kufikia sasa vituo zaidi ya 750 vinavyosimamiwa na UNICEF kwa ajili ya elimu ya watoto kambini humo vimeharibiwa na hivyo kuwanyima fursa ya masomo watoto wapatao 60,000. Takribani vituo vingine 12 vya UNICEF kwa ajili ya kuwatunzia watoto navyo vimeharibiwa.  Vyoo 600 navyo vimeathirika na vingine kuharibika na hivyo kuongeza hatari ya ugonjwa wa kuhara ambao watoto ndio wako hatarini zaidi.

Zaidi ya watoto 500,000 wa Rohingya wana mahitaji makubwa katika kambi hiyo ya Cox’s Bazar na hivyo UNICEF imeendelea kuomba dola milioni 152.5 kwa ajili ya kuunga mkono shughuli zake lakini bado pengo hadi sasa ni dola za kimarekani milioni 68.7.

WFP nayo yachukua hatua

Wakati huo huo WFP mpaka kufikia jana Julai 8, wametoa msaada wa ziada wa chakula kwa watu 6,000 walioathirika na zahma hiyo.

Msimu huu wa mvua umeanza rasmi mwezi uliopita yaani Juni lakini kulikuwa na mvua kiasi kidogo katika mwezi huo hadi ilipoanza kunyesha kwa nguvu katika mwezi huu wa Julai.

Kwa mujibu wa WFP na mamlaka ya hali ya hewa Bangladesh, hadi kufikia tarehe 7 ya mwezi huu wa Julai, kambi kubwa ya Kutupalong ilirekodi kiwango cha mvua cha hadi milimita 510 wakati kambi nyingine iitwayo Camp 16 imefikia milimita 530.

Wakimbizi 800 wamekusanywa na kuandaliwa kusaidiana na timu ya watu wa kupambana na majanga kama mafuriko na maporomoko. Mafundi wa WFP wanafanya kazi katika msimu mzima wa mvua kurekebisha na kutunza miundombinu badala ya kuanzisha miradi mipya.

Pia WFP inawaajiri wakimbizi 2,500 kila mwezi kupitia mpango wake wa fedha taslimu ili waweze kusaidia katika kazi za kupambana na majanga na kuiweka kambi katika usalama. Takribani watu 21,000 kutoka kambi za wakimbizi na jamii za wenyeji wameajiriwa kupitia mpango huu tangu mwezi Januari.

WFP inasema inagharimika dola milioni 24 za kimarekani kila mwezi kuwalisha wakimbilizi 900,000 kwa hivyo bila msaada kutoka kwa jumuiya ya kimtaifa hali inategemewa kuwa mbaya.