Msongo utokanao na ongezeko la joto utasababisha hasara sawa na kazi milioni 80 ifikapo mwaka 2030-“ILO

1 Julai 2019

Makadirio kwa kuzingatia ongezeko la joto la dunia la nyuzi joto 1.5 kufikia mwishoni mwa karne hii yanaonesha kuwa kufika mwaka 2030, asilimilia 2.2 ya jumla ya muda wa saa za kazi kote duniani itapotea kutokana na joto kali, na ni hasara sawa na nafasi za kazi milioni 80.  Maelezo zaidi na Patrick Newma

 

Hiyo ni sawa na hasara ya uchumi wa dola za kimarekani bilioni 2,400, imesema hii leo ripoti mpya ya ILO iliyotolewa mjini Geneva Uswisi.

Ripoti hiyo ya ILO iliyopewa jina kufanya kazi katika sayari yenye joto: Athari ya msongo wa joto kwa uzalishaji na kazi rasmi, imekusanya taarifa za tabianchi, saikolojia na ajira na inawasilisha makadirio ya hasara za sasa na makadirio ya hasara za uzalishaji kwa ngazi ya kitaifa, kikanda na kidunia.

Msongo wa joto ni joto la ziada zaidi ya lile ambalo mwili unaweza kuhimili bila kuathirika. Kiujumla hutokea juu ya nyuzi joto 35 katika fukuto la juu. Joto kubwa la ziada wakati wa kazi ni hatari kwa afya, linaathiri utendaji kazi na uwezo wa watu na hivyo kuathiri uzalishaji. Katika mazingira mengine hali hiyo inaweza kusababisha kiharusi kinachotokana na joto na kinaweza kuwa hatari, imefafanua ripoti hiyo ya ILO.

NASA
Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

Sekta Ambayo inategemewa kuathirika zaidi ni kilimo. Watu milioni 940 duniani kote wanafanya kazi katika sekata ya kilimo. Inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya muda wa kazi utapotea kufikia mwaka 2030 kutokana na msongo utokanao na joto. Sekta ya ujenzi nayo inategemewa kuathirika pakubwa. Sekta nyingine zinazotegemewa kuathirika iwapo hatua haitachukuliwa ni usafiri, utalii, michezo na kazi kadhaa za viwandani.

Athari za hali hii hazitakuwa na mgawanyo sawa kwani nchi zinazotegemewa kuathirika zaidi ni Asia ya kusini na Afrika Magharibi ambako takribai asilimia 5 ya saa za kazi zinategemewa kupotea kufikia mwaka 2030. Zaidi nchi zilizoko katika maeneo maskini zitaathirika zaidi. Chatherine Saget, mkuu wa kitengo cha utafiti cha ILO amesisitiza kwamba

(SAUTI YA CATHERINE SAGET)

“Athari za msongo utokanao na joto kwenye uzalishaji ni matokeo mabaya ya mabadiliko ya tabia nchi. Tunaweza kutegemea kuona kukosekana kwa usawa zaidi katika ya nchi za kipato cha chini na cha juu na kuathiri zaidi hali ya ufanyaji kazi kwa wale walioko hatarini zaidi.”

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud