Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili kufungwa kwa MINUJUSTH, Haiti

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likiijadili hali ya Haiti. Kushoto ni Jean-Pierre Lacroix na kulia ni Loune Viaud.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likiijadili hali ya Haiti. Kushoto ni Jean-Pierre Lacroix na kulia ni Loune Viaud.

Baraza la Usalama lajadili kufungwa kwa MINUJUSTH, Haiti

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumatano limekutana kujadili kuhusu kufungwa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya usaidizi wa haki nchini Haiti MINUJUSTH,  hapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Akihutubia baraza hilo mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix ameliambia baraza hilo kwamba juhudi za kuimarisha hali ya kiusalama zimezaa matokeo tofauti katika kipindi cha miezi michache iliyopita katika mazingira ya sintofahamu ya kisiasa na kusambaratika kwa serikali.

Bwana Lacroix ameeleza kwamba hakuna maandamano ya vurugu yaliyofanyika tangu siku kumi za maandamano kumalizika mwezi Februari mwaka huu ambapo watu 41 walifariki dunia na 100 kujeruhiwa.

Ameongeza kwamba vikosi vya kitaifa vya polisi vinaendelea kuonesha uwezo wake kukabiliana na vitisho dhidi ya usalama nchini humo ikiwemo kwa kupanga na kuendesha operesheni za kusaka magenge ya uhalifu kwa msaada mdogo wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Amesema kwamba, “mwisho wa ulinzi wa amani nchini Haiti unakaribia wakati mabadiliko ya hali nchini humo tangu Julai mwaka jana inadhihirisha, hali ya pandashuka ya kisiasa na udhaifu wa uchumi ,hatuwezi kupuuza hatua ambazo zimepigwa kwenye taifa hilo katika kipindi cha miaka kadhaa na hivi majuzi kuhusu kuimarisha taasisi huku vikosi vya kitaifa vya polisi vikiwa mstari wa mbele.”

Kwa mantiki hiyo mkuu huyo ameelezea msimamo wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono nia ya mamlaka Haiti kuhitimisha zhughuli za ulinzi wa amani nchini humo na wajibu wa MINUJUSTH mwezi Oktoba mwaka huu kwa kuzingatia pendekezo la mamlaka ya Haiti la kuchukua jukumu la usalama nchini kote na yote yatokanayo na hilo.

Bwana Lacroix amesema, “tuna imani na uwezo wa polisi wa kitaifa Haiti kusimamia hatari za kiusalama bila msaada wa operesheni za kimataifa. Umoja wa Mataifa utaendelea kutoa msaada wa kimawazo kwa polisi na kuimarsha uwezo wake wa vifaa ikiwemo kwa njia za msaada wa pande mbili.”

Halikadhalika amekumbusha maendekezo ya Katibu Mkuu kuendelea kushirikiana na Haiti kuimarisha ofisi zake, haki za binadamu na maarida. Kwa mujibu wa Lacroix pendekezo la kituo cha kutoa mawazo “ni muhimu katika kutimiza mahitaji ya Haiti katika hatua hii.”

Walinda amani nchini Haiti wakisaidia kuwahamisha watu baada ya kimbunga mwaka (2010)
MINUSTAH/Logan Abassi
Walinda amani nchini Haiti wakisaidia kuwahamisha watu baada ya kimbunga mwaka (2010)

 

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu licha ya hatua zilizopigwa

Kwa upande wake akihutubia kikao hicho, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bahelet amesisitiza kwamba kwamba hali nchini Haiti ni tofauti sana leo ikilinganishwa na mwaka 2004 wakati walinda amani wa Umoja wa Mataifa walipopelekwa nchini humo.

“Iwapo kiwango cha ukiukwaji wa haki za binadamu kilichotajwa wakati huo ni tofauti na hali sasa, basi changamoto kubwa ya kitaasisi inaendelea. Malalamiko ya kijamii, ufisadi na taasisi dhaifu ni vikwazo vikubwa katika kufikia haki za binadamu Haiti,” amesema Bi. Bachelet.

Kamishna Mkuu huyo amesema pia licha ya kwamba kumepigwa hatua katika utendaji kazi wa vikosi vya kitaifa vya polisi lakini kumekuwa na visa vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwmeo mauaji ya halaiki yanayoendelea kuripotiwa huku kukiwa na uwajibishwaji mdogo, “Vyombo dhaifu vya kisheria vinaathiri vibaya mfumo wa jela.”

Hatahivyo Bi.Bachelet ameelezea kutiwa moyo na ushirika wa vyama vy akiraia katika kuchagiza na kulinda haki za binadamu na kusaidia waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini akatoa anagalizo kwamba baadhi ya vyama vya kiraia vinaendelea kulengwa na kutishiwa akiongeza kwamba, “hili linapaswa kusitishwa.”

Aidha Kamishna Mkuu huyo amesemahatua zinahitaji kupongezwa lakini pia juhudi zinahitaji kuendelezwa huku akiliomba baraza la usalama, “kusaidia watu wa Haiti ili kuimarisha taasisis zao, kukabiliana na kutowajibishwa na kuimarisha na kulinda haki za binadamu kama nguzo ya uthabiti na maendeleo.”