Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tushikamane na wakimbizi kwani wanachokitaka ni amani tu:UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikutana na wakimbizi na wahamaiaji katika kituo mjini Tripoli, Libya. 4 April 2019.
UN Spokesperson/Florencia Soto Niño
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikutana na wakimbizi na wahamaiaji katika kituo mjini Tripoli, Libya. 4 April 2019.

Tushikamane na wakimbizi kwani wanachokitaka ni amani tu:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Umoja wa Mataifa umeisihi dunia kushikamana na wakimbizi ambao wamelazimika kufungasha virago kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita, mauaji , njaa na hata mateso kwani wanachokitaka ni amani.

Kupitia ujumbe wake wa siku ya wakimbizi duniani hii leo iliyobeba kauli mbiu “Hatua na wakimbizi” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema fikra zake ziko na wanawake, wanaume na watoto zaidi ya milioni 70, wakimbizi na wakimbizi wa ndani ambao wamelazimika kukimbia vita, migogoro na mateso akisema kwamba

SAUTI YA GUTERRES

 Hii ni idadi kubwa ya kushangaza -maradufu ya ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.Watu wengi waliolazimika kutawanywa wanatoka katikanchi chache tu: Syria, Afghanistan, Sudan Kusini, Myanmar na Somalia. “

Guterres ameongeza kwamba katika miezi 18 iliyopita idadi ya wakimbizi imeongezeka baada ya mamilioni zaidi ya watu kukimbia Venezuela.

Amezishukuru nchi ambazo pamoja na changamoo zake bado zimeweza kuacha wazi milango yake kukaribisha wakimbizi

SAUTI YA GUTERRES 

"Napenda kutambua utu wa nchi ambazo zinahifadhi wakimbizi hata kama zenyewe zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi na matatizo ya kiusalama.Tunapaswa kuenzi ukarimu wao kwa maendeleo na uwekezaji. Inasikitisha kwamba mfano wao haufuatwi na wote" . 

Amesisitiza kwamba ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kushughulikia tatizo la wakimbizi na hasa katika kufufua upya uaminifu  wa utawala na ulinzi wa kimataifa. Kwani amesema wakimbizi wanachokitaka zaidi ni amani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi uliopitishwa Disemba mwaka jana unatoa mwongozo wa hatua za kisasa za kuchukua kuhusu wakimbizi.

 Mamilioni ya watu kote duniani wamejiunga na kampeni ya UNHCR ya siku ya wakimbizi duniani na kuchukua hatua ziwe kubwa au ndogo kushikamana na wakimbizi.