Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya kutafuta hifadhi ni haki ya msingi ya kibinadamu: Guterres

Wasichana vigori wakitumia simu za rununu na tablet katika kambi ya waki,mbizi ya Za'atari  inayohifadhi wakimbizi wa Syria.
© UNICEF/UN051302/Herwig
Wasichana vigori wakitumia simu za rununu na tablet katika kambi ya waki,mbizi ya Za'atari inayohifadhi wakimbizi wa Syria.

Haki ya kutafuta hifadhi ni haki ya msingi ya kibinadamu: Guterres

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati duniani inaadhimisha siku ya wakimbizi duniani hii leo kwa kuwa na idadi kubwa kabisa ya wakimbizi kuwahi kurekodiwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema siku hii itumike kutafakari juu ya ujasiri wa wale wanaokimbia vita, vurugu na mateso pamoja na kutambua huruma ya wale wanaowakaribisha wakimbizi hao. 

Umoja wa Mataifa umesema jumla ya wanawake, wanaume na watoto wanaokimbia makazi yao mpaka sasa imefikia milioni 100 ikiwa ni rekodi mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema wakati leo dunia inaadhimisha siku ya wakimbizi dunia pia inathibitisha kanuni ya msingi ya kibinadamu kuwa kila mtu anahaki ya kutafuta usalama bila kujali mahali atokapo na wakati anapokimbia kusaka hifadhi.

Taarifa ya Guterres kuhusu siku hii imemnukuu akisema vita vya Ukraine vimesababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao na idadi yao ni kubwa kurekodiwa barani ulaya tangu Vita vya pili vya dunia.

Kusaka hifadhi ni haki ya msingi ya binadamu

Mkuu huyo wa umoja wa Mataifa amesema “ Sheria ya kimataifa iko wazi, haki ya kutafuta hifadhi ni haki ya msingi ya kibinadamu. Watu wanaokimbia vurugu au mateso lazima waweze kuvuka mipaka kwa usalama. Hawapaswi kukumbana na ubaguzi kwenye mipaka au kunyimwa isivyo haki hadhi ya ukimbizi au hifadhi kutokana na rangi, dini, jinsia au nchi yao ya asili.”

Akarurimana James ni mkimbizi kutoka Burundi ambaye amenufaika na ardhi iliyotolewa na serikali ya DRC kwa ajili ya wakimbizi na wenyeji wao kwa lengo la kuimarisha kujitegemea.
UN/Byobe Malenga
Akarurimana James ni mkimbizi kutoka Burundi ambaye amenufaika na ardhi iliyotolewa na serikali ya DRC kwa ajili ya wakimbizi na wenyeji wao kwa lengo la kuimarisha kujitegemea.

Amesema wasaka hifadhi hawawezi kulazimishwa kurejea katika nchi zao ikiwa uhuru wao ungali hatarini na kwamba wanapaswa kusaidiwa tena kwa heshima.

Ameenda mbali zaidi na kueleza wakimbizi sio tu wanapaswa kupatiwa hifadhi lakini pindi waingiapo kwenye nchi nyingine wanastahili kupewa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata elimu, kufanya kazi pamoja na kujiendeleza na pindi wanapoamua kurejea makwao wana uwezo wa kufanya hivyo ili kujenga upya maisha yao.

Hata hivyo amesema kubwa zaidi ni kuhakikisha maisha yao yapo salama na wanaishi kwa heshima na usalama popote pale walipo kwakuwa wakimbizi nao wanasaidia kuleta maisha mapya, ustawi, na anuwai nyingi za kitamaduni kwa jamii zinazowapokea.

Guterres amehitisha taarifa yake kwa kukumbusha umma wa ulimwengu kuwa jukumu la kulinda wakimbizi ni la kila mtu "bila kusahau ubinadamu wetu na kwamba tunapoadhimisha siku ya wakimbizi hii leo hebu tuahidi kufanya zaidi kwa ajili ya wakimbizi kila mahali na kwa nchi zinazowahifadhi huku zenyewe zikikabiliwa na msururu wa changamoto. Tusimame pamoja kwa mshikamano. Tutetee uadilifu wa mfumo wa ulinzi wa kimataifa.”