Siku ya wakimbizi ni siku ya kutambua utu kwa vitendo: Grandi

20 Juni 2018

Siku ya wakimbizi duniani ni siku ya kutambua utu kwa vitendo na pia kushikamana na wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, amesema Kamishina mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa Filippo Grandi. 

Grandi ambaye pia ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudimia wakimbizi,  UNHCR ametoa kauli hiyo katika ujumbe maalumu wa siku ya wakimbizi duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 20,  na kusisitiza kuwa wakati migogoro inazuka, inajirudia, inaendelea na kushika kasi zaidi watu milioni 68 wametawanywa duniani kote na kwamba

“Watu 9 kati ya 10 wako katika nchi zao au nchi jirani na athari zake ni kubwa sana kwa wakimbizi wenyewe  na kwa jamii zilizofungua milango yake kuwapokea , na sasa kuliko wakati mwingine wowote, kuwahudumia wakimbizi ni lazima uwe ni wajibu wa kimataifa na wa pamoja ni wakati wa kufanya mambo tofauti”

Ameongeza kuwa nchi na jamii zinaochukua jukumu la kuzisaidia familia zilizotawanywa na machafuko, zinahitaji mfumo maalumu wa msaada na wa muda mrefu na wakimbizi wanahitaji kujumuishwa katika jamii mpya ili waweze kupata fursa ya kudhihirisha mchango wao, na mkakati mpya wa kimataifa kwa ajili ya wakimbizi utakaopitishwa mwaka huu unanuia kutimiza azma hii kwa sababu

“Kuwa na sheria na sera stahiki ni muhimu sana, lakini ni watu na jamii zilizo mstari wa mbele wakati wakimbizi wakiwasili na zile zinazowakaribisha ndizo zinazoleta tofauti kubwa, tofauti kati ya kukataliwa na kujumishwa, baina ya kukata tamaa na kuwa na matumaini na baina ya kuachwa nyuma na kujenga mustakhbali wao.”

Amesema kupitia ukarimu wao wanaangaza nuru na fursa zizizo na mipaka kwa wakimbizi, kwani kuwasaidia wakimbizi kujenga upya maisha yao ni jukumu la kila mtu hivyo siku ya leo ni ya changamoto ya kutambua utu kwa vitendo na kuungana na watu hao kwa msaada, iwe mashuleni, makanisani, maeneo jirani na hata mahali pa kazi kwani mshikamano ndiko unakoanzia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter