Fedha zaidi na utashi wa kisiasa kutoka pande zote DRC ni muarobaini wa kutokomeza Ebola- Dkt.Tedros

20 Juni 2019

Mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC utatokomezwa kabisa pale utashi wa kisiasa kutoka pande zote sambamba na ushiriki wa dhati wa jamii vitakaposhika hatamu sambamba na shirika hilo kupatiwa fedha za kutosha.

Ni kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus aliyotoa leo mjini Geneva, Uswisi wakati wa akizungumzia na nchi wanachama wa shirika hilo kufuatia ziara yake huko DRC na Uganda alikojionea hali halisi ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao sasa umeshaua zaidi ya watu 2100 tangu ulipuke mwezi Agosti mwaka jana.

“Utashi wa kisiasa ni lazima utoke pande zote za uongozi wa kisiasa nchini DRC,” amesema Dkt, Tedros akiongeza kuwa ni kwa kufanya hivyo jamii nazo zitaelewa kuhusu tishio la Ebola na kubeba jukumu la kumaliza mlipuko huo.

Amezungumzia pia ukata unaokumba shirika hilo kwenye operesheni dhidi ya Ebola akisema, “WHO inahitaji dola milioni 98 ambazo kati ya hizo dola milioni 44 ndio zimepatikana hadi sasa na kuacha pengo la dola milioni 54.”

Dkt. Tedros amesema iwapo fedha hizo  hazitapatikana, “WHO itashindwa kuendeleza kasi yake ya sasa ya kudhibiti ugonjwa huo . Wadau wengine wamepunguza wigo wa operesheni zao au hata kuacha kabisa kutokana na ukata.”

Hata hivyo kinachomtia moyo mkuu huyo wa WHO kutokana na ziara yake ya 9 huko DRC ni mwitikio kutoka pande zote za kisiasa, yaani upande wa serikali na upinzani pamoja na wadau wengine ambao kwa pamoja waliahidi kutekeleza wajibu wao ili jamii ielewe hatari za ugonjwa huo.

Pamoja na utashi wa kisiasa na jamii kushiriki, mahitaji mengine muhimu yalitajwa ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira ya kiusalama pamoja na kuhakikisha kuwa chanjo dhidi ya Ebola inatumika vizuri kwa kuwa imekuwa mbinu thabiti ya kukinga wale wote waliobainika kuwa na mgusano na wagonjwa wa Ebola.

 

TAGS: Ebola, DRC, Uganda, Dkt. Tedros Ghebreyesus, WHO

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud