Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya ni mfano wa mafanikio ya huduma ya afya kwa wote- Dkt. Tedros

Mama na mwana wapewa chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa  kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.
UNICEF/ Nangyo
Mama na mwana wapewa chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.

Kenya ni mfano wa mafanikio ya huduma ya afya kwa wote- Dkt. Tedros

Afya

Mkutano wa 72 wa Baraza la shirika la afya duniani, WHO umeanza leo mjini Geneva, Uswisi ukilenga kutathmini mwelekeo wa afya duniani na harakati za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs hususan yale yahusuyo afya.

Akifungua mkutano huo wa siku 9, Mkurugenzi Mkuu wa WHO  Dkt. Tedros Ghebreyesus amewataka wajumbe siyo tu kujadili bali pia kusikiliza sauti za wale ambao hawapo kwenye chumba cha mkutano.

“Tunapaswa kusikiliza sauti za wale wasiopo hapa, wale ambao hawana sauti. Wale ambao wameachwa nyuma, ni wao ambao tunawahudumia,” amesema Dkt.Tedros.

Amegusia pia mafanikio yaliyopatikana tangu kikao kilichopita cha mwaka jana, akisema mwaka 2018 ulikuwa na mafanikio ya aina yake ikiwemo kwa mara ya kwanza dunia imefikia maendeleo makubwa ya huduma ya afya kwa wote.

“Mwaka jana nimetaja mpango wa Kenya wenye matamanio makubwa ya kutekeleza mpango mpya wa huduma ya afya kwa wote, kwa usaidizi wa WHO. Mwezi Disemba, nilipata heshima kubwa ya kuwepona Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kuzindua mpango huo huko Kisumu. Tayari mpango huo unazaa matunda,” amesema Dkt. Tedros.

Amemtolea mfano Immaculate Otene, mama wa watoto wanne na mwenye umri wa miaka 33 akisema “Immaculate hana ajira, na mume wake mara nyingi hana kazi. Lakini mpango wa huduma ya afya kwa wote nchini Kenya ulioandaliwa kwa msaada wa WHO, umewezesha familia yake kuweza kupata huduma bure ya afya.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa afya amesema kwa kutambua tu kuwa wanaweza kupata huduma bure ya afya wakati wowote, Immaculate hana tena hofu wala wasiwasi ambao yeye na mumewe wamekuwa wakipata akimnukuu akisema kuwa, “familia yangu yote sasa imesajiliwa naweza kumpeleka mtoto wangu yoyote hospitali bila wasiwasi.”

Mtoto manusura wa Ebola aitwaye Muhindo akichunguzwa macho  yake na Dkt. Steven Yeh
WHO/J. D. Kannah
Mtoto manusura wa Ebola aitwaye Muhindo akichunguzwa macho yake na Dkt. Steven Yeh

Kwa mujibu wa Dkt.  Tedros, simulizi kama ya Immaculate zinapatikana pia India, Afrika Kusini, Ufilipino, Misri na kwingineko akisema kuwa ni kwasababu ya azimio la Astana ambalo liliridhiwa na nchi 194 ya kwamba hakuwezi kuwepo na huduma ya afya kwa wote bila huduma ya afya ya msingi.

“Ni kwa kupitia huduma thabiti ya afya ya umma ambapo nchi zinaweza kuzuia, kubaini na kutibu magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Ni kwa kupitia huduma thabiti ya afya ya umma ambapo milipuko ya magonjwa inaweza kubainika na kudhibitiwa kabla haijawa tishio, » amesema Dkt. Tedros.
 
Mafanikio mengine ni kuanza kutolewa kwa chanjo ya dhidi ya Malaria nchini Malawi akitaja pia mataifa ambayo yamefanikiwa kutokomeza Malaria kuwa ni Uzbekistan na Paraguay  huku akisema katika mkutano wao wa sasa Argentina na Algeria zitatangazwa kuwa zimetokomeza Malaria.

Amezungumzia pia Ebola akisema ni moja ya milipuko ambayo wanaendelea kukabiliana nayo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akisema hadi sasa wamepatia chanjo zaidi ya watu 120,000.

Hata hivyo amesema wanachopambana nacho DRC si virusi vya Ebola pekee bali pia ukosefu wa usalam, ghasia na ukosefu wa taarifa sahihi pamoja na kutoaminiana sambamba na masuala ya kisiasa kujumuishwa kwenye harakati dhidi ya mlipuko huo.

Mkurugenzi huyo mkuu wa WHO ametumia mkutano huo kutangaza mabalozi wema wapya wanne wa kusaidia kusongesha afya duniani ambapo mmoja wao ni Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirlef na atakuwa balozi mwema wa afya pahala pa kazi.

Wengine ni Alisson Becker, golikipa wa timu ya taifa ya wanawake ya soka nchini Brazil na pia timu ya Liverpool pamoja na Dkt. Natália Loewe Becker, daktarin wa Brazil ambao wao watajikita kwenye kusongesha afya. Mwingine ni Cynthia Germanotta, Rais wa taasisi ya Born This Way aliyoiasisi pamoja na mwanae Lady Gaga na atakuwa balozi mwema wa afya ya akili.