Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya utesaji binadamu na ukiukwaji wa haki Comoro kuangaziwa

Mkazi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro
UN Environment/Hannah McNeish
Mkazi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro

Hali ya utesaji binadamu na ukiukwaji wa haki Comoro kuangaziwa

Haki za binadamu

Masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu hususan watu kuteswa kinyume cha kanuni nchini Comoro yatamulikwa na kufanyiwa tathmini wakati wa ziara ya wiki moja ya mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utesaji, Nils Melzer.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imesema ziara hiyo inayoanza Kesho Jumatano itatoa fursa kwa mtaalamu huyo kutathmini na kubaini changamoto juu ya hatua za kuzuia utesaji na aina nyingine ya ukatili pamoja na adhabu zisizo na utu.

“Kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Azali Assoumani wa Comoro mwezi Machi mwaka huu, jukumu langu la msingi ni kuzungumza na watoa maamuzi na wadau wengine muhimu ili kusaidia mamlaka kuzingatia utawala wa sheria na kuchunguza na kufungulia mashtaka madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi, mateso na manyanyaso wakati wa uchaguzi na baada,” amesema Bwana Melzer.

Mtaalamu huyo amesema pia ana taarifa kuhusu changamoto ambazo serikali ilikumbana nazo wakati idadi kubwa ya raia walijaribu kuondoka visiwa vya Comoro kwa kutumia boti zisizo salama ili kuelekea kisiwa cha jirani cha Mayotte, lakini walirejeshwa na mamlaka za Ufaransa.

Akiwa nchini humo, mtaalamu huyo atakuwa na mazungumzo na mamlaka za Comoro, mahakama, mamlaka za kitaifa za haki za binadamu, mashirika ya Umoja wa Mataifa, manusura wa utesaji na familia zao na pia atatembelea maeneo yanayoshikilia watu kwenye visiwa vya Comoro Ku una Anjouan.

Ziara hii inafuatia ahadi ya serikali ya Comoro ya mwezi Januari mwaka huu ya kuwa tayari kupokea wataalamu wote wenye majukumu kuhusu haki.