Mtaalamu huru asitisha ziara yake Comoro

18 Juni 2019

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu utesaji, Nils Melzer, amesitisha ziara yake aliyokuwa afanye Comoro, baada ya kukumbwa na vizuizi vya hapa na pale.

Ziara hiyo ya wiki moja ililenga , kutoa fursa kwa mtaalamu huyo kutathmini na kubaini changamoto juu ya hatua za kuzuia utesaji na aina nyingine ya ukatili pamoja na adhabu zisizo na utu.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCRC, imemnukuu Bwana Melzer akielezea masikitiko yake kuwa alishindwa kufikia kwa uhuru watu wote ambao alihisi ni muhimu ili kukamilisha jukumu lake.

Mathalani, Melzer aliweza kufanya ziara aliyopanga kwenye rumande moja huko Comoro Kuu lakini ziara yake kwenye maeneo matatu yaliyo chini ya polisi na mahakama huku Moroni na kisiwa cha Anjouan zilizuiliwa.

 “Hili linatia hofu sana kwa sababu nilikuwa nimepokea ushahidi mahususi wa madai ya vitisho, matumizi ya nguvu kupita kiasi na utendawaji mbaya wa watuhumiwa,” amesema Bwana Melzer.

Amesema ni dhahiri kuwa mamlaka  husika hazikuwa zimefanya maandalizi yanayotakiwa ya kuwezesha ziara hiyo kwa muijbu wa hadidu za rejea zilizoandaliwa upya kwa ajili ya wataalamu hao, hadidu za rejea ambazo ziliwasilishwa rasmi kwa serikali miezi kadhaa iliyopita.

Mtaalam huyo ametolea mfano kuwa kando ya baadhi ya maeneo ambayo yalichaguliwa awali kwa ajili ya ziara yake, mamlaka husika kwenye maeneo ya rumande hazikuwa zimearifiwa na wizara husika kwa hiyo, “hazikuwa kwenye nafasi ya kunipatia fursa ya ziara.”

Halikadhalika amesema alizuiwa kukamilisha mahojiano na watu wanne kati ya watano wanaoshikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi huko Anjouan, “kwa madai kwamba sikuwa nimeomba kibali kutoka kwa kila jaji anayehusika na mtuhuiwa niliyetaka kumhoji.”

Bwana Melzer amesema licha ya mkutano usio rasmi na Wizara ya Mambo ya Nje wa kutaka kutatua sintofahamu iliyotokea,hakuna maelezo rasmi ambayo yaliwasilishwa.

“Tarehe 15 Juni, ikiwa ni nusu ya ziara yangu, nilihitimisha kuwa kimaadili, ziara hiyo niliyoanza tarehe 12 Juni na ilikuwa imalizike tarehe 18 Juni imekumbwa na rabsha kiasi kwamba ninalazimika kuisitisha,” amesema Bwana Melzer.

Mtaalamu huyo ameshukuru serikali ya Comoro kwa kumwalika kufanya ziara hiyo rasmi, ya pili kufanywa na mtaalamu huru.

Hata hivyo amesisitiza kuwa ziara za namna hiyo zinahitaji kujitolea kwa dhati kwa upande wa mwalikwa  sambamba na maandalizi upande wa waalikaji ili ziara iweze kuwa na mantiki na ikidhi vigezo vya kimataifa na hadidu za rejea.

Mtaalamu huyo amesema wiki ijayo atawasilisha ripoti yake ya awali na ataendelea kuwasiliana na serikali ya Comoro na wasuluhishi huku akisema ripoti yake kamili atawasilisha mbele ya Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwakani.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Hali ya utesaji binadamu na ukiukwaji wa haki Comoro kuangaziwa

Masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu hususan watu kuteswa kinyume cha kanuni nchini Comoro yatamulikwa na kufanyiwa tathmini wakati wa ziara ya wiki moja ya mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utesaji, Nils Melzer.