Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalamu aonya vifungo vya muda mrefu vya upweke kwenye gereza la Connecticut nchini Marekani

Profesa Nils Melzer, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mateso, akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani 16 Oktoba 2018
UN Photo/Eskinder Debebe)
Profesa Nils Melzer, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mateso, akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani 16 Oktoba 2018

Mtaalamu aonya vifungo vya muda mrefu vya upweke kwenye gereza la Connecticut nchini Marekani

Haki za binadamu

Mtaalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake juu ongezeko la matumizi  ya vifungo vya upweke na vya muda mrefu kwenye magereza nchini Marekani.

Nils Melzer ambaye ni mtaalamu maalum kuhusu mateso, amesema kuwa, “kwa miaka kadhaa ofisi ya haki za binadamu uimekuwa ikielezea wasiwasi wake duniani kote juu ya vifungo vya upweke ambavyo vimeenea na ni vya kiholela. Mtangulizi wangu Profesa Juan Mendez amekuwa akielezea dhahiri ni kwa vipi kitendo hicho kinaweza kuwa mateso.”

Bwana Melzer amezungumzia kisa cha hivi karibuni zaidi kwenye gereza la Connecticut ambako “gereza hilo limekuwa likitumia adhabu za shinikizo na mateso na kwa muda mrefu ikiwemo kuwatenga wafungwa moja kwa moja, wafungwa kufungwa minyororo hata ndani ya vyumba vyao. Kunaonekana kuna sera ya jimbo ya kuwapatia wafungwa machungu kimwili na kiakili, vitu ambavyo vinaweza kuwa ni mateso.”

Mtaalamu huyo amesema mazingira hayo ya kikatili ambavyo wakati mwingine hutambuliwa nchini Marekani kama kutengwa, nyumba salama au shimo hutumika sana nchini humo hususan kwa wafungwa wanaotambuliwa kama wa hatari zaidi kutokana na awali kushirikiana na magenge ua kihalifu.

Amekumbusha kuwa, matokeo ya mateso kama hayo mara nyingi hayawezi  kutibika na wakati mwingine husababisha mtu kujiua.

Amekumbusha kuwa kutumia vifungo vya kutengwa kwa watu wenye ulemavu wa kiakili au kimwili hairuhusiwi chini ya sheria za kimataifa na kwamba hata kama inaruhusiwa na sheria ya nchi bado inakatazwa na sheria za kimataifa kwa mujibu wa kanuni za Mandela.

Kanuni za Mandela zilizorekebishwa mwaka 2015, ni kanuni zinazotumiwa na Umoja wa Mataifa zikiainisha kifungo cha kutengwa kuwa ni mfungwa kutengwa peke yake kwa saa 22 au zaidi kwa siku bila mawasiliano yoyote ya maana ya ubinadamu. Kifungo cha kutengwa kwa mujibu wa kanuni  hizo kinaweza kutumika katika mazingira ya kipekee na kifungo cha kutengwa cha zaidi ya siku 15 mfululizo huonekana kuwa ni mateso.

Mtaalamu huyo  maalum anatarajiwa kuwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la  Umoja wa Mataifa hii leo na kuzungumza na waandishi wa habari tarehe 2 mwezi ujao huko Geneva, Uswisi.