Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi na wadau jiepusheni na matendo yanayoweza kuuvuruga usalama zaidi wa Comoro- Guterres.

Rais wa Muungano wa visiwa vya Comoro Azali assoumani akuhutubia wakati wa kikao cha 73 cha Baaraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York mwaka 2018.
UN Photo/Cia Pak
Rais wa Muungano wa visiwa vya Comoro Azali assoumani akuhutubia wakati wa kikao cha 73 cha Baaraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York mwaka 2018.

Viongozi na wadau jiepusheni na matendo yanayoweza kuuvuruga usalama zaidi wa Comoro- Guterres.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumzia taarifa iliyotolewa na mahakama kuu ya Comoro kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais na viongozi wa majimbo uliofanyika tarehe 24 Machi 2019, akizitaka pande zote husika kuepusha machafuko zaidi na kutatua tofauti zao kisheria na kwa njia ya amani.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake jijini New York Marekani, Bwana Guterres ameeleza kusikitishwa kwake na ripoti za vurugu na vifo pamoja na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa ikiwa ni pamoja na vizuizi kwa vyombo vya habari. Katibu Mkuu amesisitiza kwamba utawala wa sheria na kuheshimu haki za msingi lazima vizingatiwe. Bwana Guterres amezisihi mamlaka za Comoro na wadau wengine kujiepusha na matendo yoyote yanayoweza kuifanya hali ya sasa kuwa mbaya zaidi na kuwataka wachukue hatua kwa kuzingatia sheria na haki za binadamu.

Kwa mujibu wa duru za habari kisiwa cha Comoro ambacho kimepitia zaidi ya majaribio 20 ya mapinduzi kimekuwa na utaratibu kwa miaka mingi wa marais wa mzunguko katika visiwa vyote  vinavyounda Comoro ambavyo ni Anjwani, Meheli, Mayote na Grand Comoro. Na purukshani za baada ya uchaguzi wa juma lililopita kwa mujibu wa tarifa za serikali zimesababisha vifo vya watu watatu na wengine wengi kujeruhiwa katika mozozo wa kupinga kuchaguliwa tena Rais Azali Assoumani.

Aidha Bwana Guterres amerejelea wito uliotolewa na Muungano wa Afrika AU mnamo tarehe 29 mwezi Machi na kuungwa mkono na Muungano wa Ulaya, (EU)na pia kamisheni ya bahari ya hindi (Indian Ocean Commission) ya kuwa na mjadala wa pamoja chini ya uongozi wa Muungano wa Afrika AU. Pia amerejelea ahadi ya utayari wa Umoja wa Mataifa kusaidia juhudi za kukuza umoja wa kitaifa, amani, utulivu na maendeleo katika umoja wa visiwa vya Comoro.