Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde, Finland tumia urais wa EU kuboresha mustakabali wa wasaka hifadhi  Ulaya- UNHCR

Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea
Frontex/Francesco Malavolta
Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea

Chonde chonde, Finland tumia urais wa EU kuboresha mustakabali wa wasaka hifadhi  Ulaya- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, leo limewasilisha mapendekezo yake kwa Finland ili ishinikize kwenye Baraza la Muungano wa Ulaya hoja ya marekebisho ya  kusaka hifadhi.

Hatua hiyo inazingatia kuwa Finland itachukua Urais wa Baraza hilo kuanzia tarehe Mosi mwezi ujao, wakati huu ambapo kuna mjadala wa bajeti na mashauriano yatakayoongoza kazi za Muungano wa Ulaya, EU kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Mwakilishi wa  UNHCR kanda ya Ulaya Gonzalo Vargas Llosa, amesema mapendekezo hayo yamejikita katika vipaumbele  vya dharura ambavyo ni kujenga ushirikiano na mshikamano na wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, na pia kushinikiza njia thabiti kwa nchi wanachama wa EU kuwajibika pamoja katika suala la wasaka hifadhi.

“EU ina fursa ya kipekee ya kusonga mbele na kufanya marekebisho ambayo ni muhimu na ambayo hayawezi kusubiri tena,” amesema Vargas Llosa ambapo amesema hadi pale kutakapokuwepo na mfumo bora wa usimamizi na ulinzi, shirika hilo linatoa wito kwa nchi wanachama kugawana majukumu ya watu wanaowasili baada ya kuokolewa kwenye bahari ya Mediteranea.

Mapendekezo pia yanatoa wito kwa EU kuonyesha uongozi duniain kwa kupanua mpango wake wa kupokea wakimbizi wanaohamishiwa nchi ya tatu, sambamba na njia zingine halali za kupokea wakimbizi.

Mvulana akitembea  ndani ya kambi ya Calais, kaskazini mwa Ufaransa. Takwimu zinaonyesha kuwa  takribani wahamiaji 900 na wasaka hifadhi wanaishi eneo hili bila vyoo wala huduma za kujisafi.
UNICEF/Geai
Mvulana akitembea ndani ya kambi ya Calais, kaskazini mwa Ufaransa. Takwimu zinaonyesha kuwa takribani wahamiaji 900 na wasaka hifadhi wanaishi eneo hili bila vyoo wala huduma za kujisafi.

Ni kwa mantiki hiyo, UNHCR inasihi Finland wakati wa urais wake iunge mkono mkakati wa kimataifa uliotungwa na shirika hilo na wadau wake wa kupunguza pengo kati ya fursa za uhamiaji nchi ya tatu na mahitaji.

“Kadri fursa halali zinapofunguka, ndivyo watu wachache zaidi wataweza kuweka hatarini maisha yao wakisaka maeneo salama ya kuishi barani Ulaya,” amesema Vargas Llosa.

Kipaumbele cha tatu ni kwa Finland kusongesha katika nchi zote za EU suala la kuondokana na watu kutokuwa na utaifa ambapo mwakilishi huyo wa UNHCR kanda ya Ulaya amesema, “kuna njia ambazo zimedhihirika za kubaini na kulinda watu wasio na utaifa na mataifa mengi zaidi yaridhia njia hizo ikiwemo kuzuia watoto kuzaliwa bila utaifa.”

UNHCR imesema kwa upande wake iko tayari kusaidia Finland wakati wa kipindi cha urais wa Baraza la EU, EU yenyewe na nchi wanachama wakati wanafanya kazi kuimarisha mshikamano na wakimbizi nan chi zinazowahifadhi kote duniani.