Libya tuko tayari kuwasaidia mbinu mbadala ya kushikilia wasaka hifadhi - UNHCR

5 Machi 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema liko tayari kusaidia Libya kuandaa maeneo mbadala ya kushikilia wasaka hifadhi badala ya vituo vya korokoroni ambavyo vimekuwa kero na kusababisha kiwewe miongoni mwa wasaka hifadhi hao.

Kauli hiyo ya UNHCR imetolewa leo huko Geneva, Uswisi na msemaji wake Shabia Mantoo kufuatia tukio la wiki iliyopita ambapo wasaka hifadhi wanaoshikiliwa kwenye kituo cha Sikka kwenye mji mkuu Tripoli walifanya vurugu wakipinga mazingira duni na magumu kwenye kituo hicho na bila kuwepo kwa dalili zozote za kuhamishiwa nchi nyingine.

Yaelezwa kuwa takribani watu 50 walijeruhiwa kwenye tafrani hiyo wakati polisi walipowasili ili kuwatuliza na wawili kati ya majeruhi walihamishiwa hospitali ya Abu Slim.

Bi. Mantoo amesema kinachotia hofu zaidi ni kwamba licha ya kuelezea wasiwasi wao mbele ya mamlaka juu ya hali za watu hao, mpaka sasa hawajaweza kupata fursa ya kukutana na waathirika wa tukio hilo, zaidi ya fursa ya jumapili ya kufika kwenye kituo hicho ili kuwahamishia watu hao kwenye kituo cha kusubiria kuondoka.

UNHCR inasisitiza wito wake kwa mamlaka nchini Libya kuacha kitendo cha kuwashikilia korokoroni wasaka hifadhi na badala yake iko tayari kusaidia mamlaka hizo kupata maeneo mbadala ya kuhifadhi watu hao.

Hii ni mwaka uliopita, 2017, wahamiaji wa Nigeria waliokuwa wamekwama nchini Libya, walipotua Lagos Nigeria kwa msaada wa IOM.
IOM
Hii ni mwaka uliopita, 2017, wahamiaji wa Nigeria waliokuwa wamekwama nchini Libya, walipotua Lagos Nigeria kwa msaada wa IOM.

Wakati wa tukio hilo zaidi ya wasaka hifadhi 400 walikuwemo kwenye kituo hicho wakiwemo waetritrea 200, wasomali 100, waethiopia 53 na wasudan 20.

Mwezi Disemba mwaka jana, UNHCR kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya, ilifungua kituo cha kuwakusanya na kuhifadhi wasaka hifadhi tayari kwa ajili ya kuongeza kasi ya mchakato wa kuhamishiwa nchi nyingine.

Hata hivyo, kutokana na kupungua kwa fursa za maeneo ya kuhamishiwa, idadi kubwa ya wakimbizi wameendelea kusalia  kwenye vituo vya korokoroni kwa muda usiojulikana, hali iliyosababisha kiwewe miongoni mwao.

Jana pekee, UNHCR ilihamisha wakimbizi 128 kuelekea Niger, na hii ni safari ya tatu ndani ya mwaka huu na imefanya idadi ya waliohamishwa mwaka huu pekee kutoka Libya kufikia 3,303.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter