Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka kuimarishwa kwa utafutaji na uokoaji bahari ya Mediterenea

Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea
Italian Coastguard/Massimo Sestini
Waokoaji wa kikosi cha wanamaji cha Italia wakiokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediteranea

UNHCR yataka kuimarishwa kwa utafutaji na uokoaji bahari ya Mediterenea

Wahamiaji na Wakimbizi

Watafuta hifadhi  45,700  na wahamiaji wamefikia pwani ya Ulaya baada ya kuvuka bahari ya Mediteranea katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2018.

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR inasema  hii ni idadi ndogo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2016, ingawa idadi ya vifo imeongezeka. Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Charlie Yaxley amewaambia waaandishi wa habari kuwa wanasikitishwa na idadi kubwa ya wanaume, wanawake na watoto wanaoendelea kufamaji katika bahari, na kwa idadi kubwa. Tayari mwaka 2018, idadi ya waliopoteza maisha au wasiojulikana waliko imefika  zaidi ya 1,000 kwa mwaka wa tano mfululizo, licha ya kupungua kwa wanaovuka kuelekea Ulaya. Kwa mantiki hiyo amesema kuongezeka kwa vifo kunaonyesha umuhimu wa  kuimarisha uwezo wa kutafuta na kuokoa watu wanaovuka bahari. Hata hivyo amesema UNHCR imetoa shukrani kwa wale wanaohusika na shughuli za uokoaji lakini kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za bahari na kuruhusu juhudi za kuitikia wito wa watu walio hatarini kwenye bahari.Amesema wakati huu ambapo ndio kipindi cha idadi kubwa ya wasaka hifadhi kuvuka bahari hiyo, ni lazima suala la kuokoa maisha lipatiwe kipaumbele. Bwana Yaxley amesema kupunguza uwezo wa kutafuta na uokoaji kutasababisha upotevu usiohitajika wa maisha, wakati wasafirishaji haramu wakiendelea kusafirisha watu kwa kutumia vyombo visivyofaa. UNHCR imerejelea  wito wake wa wiki za hivi karibuni, uliotolewa pamoja na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, kuomba ushirikiano wa kikanda juu ya muongozo wa kuvuka  bahari ya Mediteranea, ambayo inatoa muongozo kuhusu utafutaji na uokoaji.