Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaendelea kuwasaidia watu wa Iran baada ya mafuriko makubwa

Moja ya nyumba zilizoathirika na mafuriko katika jimbo la Golestan nchini Iran na kusababisha zaidi ya watu 366.000 kuyakimbia makazi yao,
NRC/Hamidreza Fakhar
Moja ya nyumba zilizoathirika na mafuriko katika jimbo la Golestan nchini Iran na kusababisha zaidi ya watu 366.000 kuyakimbia makazi yao,

UN yaendelea kuwasaidia watu wa Iran baada ya mafuriko makubwa

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa unaendelea kuwasaidia watu wa Iran tangu kutokea kwa mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zilizoanza kunyesha tarehe 19 mwezi Machi mwaka huu  ambapo kwa wiki kadhaa majimbo 25 kati ya 31 nchini humo yaliathirika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Iran, serikali ya Iran inakadiria madhara ya mafuriko katika sekta ya afya kuwa ni takribani dola milioni 300 na takribani dola bilioni 1.5 kwa upande wa kilimo, hata hivyo takwimu hizo zinaweza kuongezeka.

Ingawa maonyo ya mapema na uhamishaji watu vilivyofanywa na serikali ya Iran vilisaidia kuokoa maisha ya wengi, lakini makazi milioni 1.8 yaliathirika. Umoja wa Mataifa unazisaidia juhudi za serikali ya Iran kufanya tahmini ya mahitaji ya makazi na pia mahitaji baada ya janga hilo.

halikadhalika, Umoja wa Mataifa umekuwa ukiisaidia serikali na watu wa Iran tangu kuanza kwa janga hili. Hadoi kufikia sasa Umoja wa Mataifa umetoa vifaa tiba vya dharura, vifaa vya afya ya uzazi, chanjo, mahitaji ya afya za wanawake, makazi ya dharura, vifaa vya ndani na vifurushi vya chakula.

Baada ya msaada wa haraka wa kuokoa maisha, Umoja wa Mtaifa na jumuiya ya kimataifa, wanaendelea kuuunga mkono juhudi za serikali kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu kuzuia na kudhibiti madhara ya majanga ya asili.

Mpango wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa unawalenga watu 115,000 walioathirika zaidi na katika upande wa sekta ya afya, Umoja wa Mataifa unasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kiafya na za kuokoa maisha zikiwemo huduma za afya ya uzazi.

Kwa upande wa elimu, Umoja wa Mataifa unahakikisha wanafunzi wanaendelea na elimu yao pamoja na kuwapatia msaada wa kisaikolojia.

Vile vile Umoja wa Mataifa unasimamia kuhakikisha huduma za maji safi na salama, pamoja na iundombinu ya kujisafi vinarejea.

Pia suala la usalama linaangaziwa ili kuhakikisha watu walioathirika wanapata msaada wa kisaikilojia na pia wasichana na wanawake wanapata usaidizi kulingana na mahitaji yao mahususi.

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Iran Bi Ugochi Daniels, katika mkutano na serikali pamoja na jumuiya ya kimataifa ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa,“tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kwa msaada wenu huu wa ukarimu ili kutekeleza mpango huu wa usaidizi.”