Chonde chonde dunia haiwezi kumudu vita vingine Ghuba:Mkuu wa UN

3 Januari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake na kutoa wito wa kupunguza mvutano katika eneo lote la Ghuba  baada ya kuuawa kwa jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Iran katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani nchini Iraq.

António Guterres katika taarifa yake iliyotolewa Ijumaa asubuhi na  msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, imesema kwamba mkuu huyo wa UN "alikuwa anatetea mara kwa mara akichagiza kupunguza mvutano ", na kuongeza kuwa "huu ni wakati ambao viongozi lazima watulie zaidi na kujizuia na machafuko.

Mkuu wa Kikosi cha Wakurdi cha Iran, Jenerali Qasem Soleimani, alilengwa na kuuawa nje ya uwanja wa ndege wa Baghdad, katika shambulio la anga ambalo liamriwa na Rais wa Merekani, Donald Trump, kulingana na taarifa iliyotolewa na Idara ya Ulinzi ya Marekani.

Katibu Mkuu Guterres- Huu ni wakati ambao viongozi wanapaswa kujizuia na mvutano Zaidi. dunia haiwezi kumudu vita vingine Ghuba.

Kiongozi wa wanamgambo wa Iraqi Abu Mahdi al-Muhandis, alikuwa pia miongoni mwa wale waliouawa wakati wa shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari.

Kundi lake la Kataib Hezbollah lililaumiwa na Marekani kwa shambulio la roketi ambalo lilimuua mkandarasi wa kiraia wa Merekani nchini Iraq wiki iliyopita, na aliongoza kundi la wanamgambo ndani ya Iraqi, lililohusiana na Iran.

Kwa mujibu wa duru za Habari Kiongozi mkuu wa Iran, Ayattollah Ali Khamenei, ametoa taarifa akitaka siku tatu za maombolezo ya umma kufuatia kifo cha Jenerali Soleimani na kusema kutalipwa kisasi dhidi ya mashambulizi hayo ya Marekani.

Mwakilishi maalum wa UN Iraq

Naye mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa Iraq UNAMI Hennis-Plesshaert akikubaliana na tarifa ya Katibu Mkuu amesema kwambaendapo viongozi katika ukanda huo wa Ghuba hawatojiuzuia na mvutano zaidi matokeo yake yanaweza mzunguko mwingine mbaya wa machafuko.”

Kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema kwa muda mrefu Iraq imekuwa uwanja wa mashindano tofauti ya wenye uwezo. Iraq inastahili utulivu na amani, na vichwa vilivyotulia lazima vishinde.”

Katika mlolongo wa ujumbe wa twitter mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji na mauaji ya kupangwa Agnes Callamard amehoji uhalali wa mashambulio hayo ya anga ya Marekani chini ya sheria za kimataifa na kuutaka Umoja wa Mataifa kutumia jukwaa na nyezo za kisheria ilizonazo kuingilia kati suala hili. “Hakuna wakati mwingine wowote wa muhimu na wa shinikizo kwa Umoja wa Mataifa na uongozi wake kama sasa.”

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud