Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunisia na Niger ‘kidedea’ uchaguzi wa Baraza la Usalama

Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifajijini New York Marekani
UN/Eskinder Debebe
Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifajijini New York Marekani

Tunisia na Niger ‘kidedea’ uchaguzi wa Baraza la Usalama

Masuala ya UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limechagua nchi tano wanachama wa umoja huo ambao watachukua ujumbe usio wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzia mwezi Januari mwakani.

Uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 23 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na kanuni namba 142 ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu chaguzi za kila mwaka za wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka miwili.

Kanuni zinataka mshindi apate theluthi mbili za kura ambapo hii leo kwa upande wa bara la Afrika, nchi zilizochaguliwa ni Niger na Tunisia ambazo zitachukua nafasi ya Cote d’Ivoire na Equatorial Guinea zinazomaliza muda wao mwishoni mwa mwaka huu.

Kutoka kundi la Asia-Pasifiki, kiti kilichokuwa kinashindaniwa ni kimoja ambapo Vietnam imeshinda na itachukua nafasi ya Kuwait.

Kwa upande wa kundi la nchi za Amerika ya Kusini na Karibea, Saint Vincent na Grenadines imeibuka kidedea kwa kupata kura 185 dhidi ya El Salvador iliyopata kura 6 na hivyo kuchukua nafasi ya Peru inayomaliza muda wake.

Nafasi ya bara la Ulaya imechukuliwa na Estonia iliyopata kura 132 ambayo imezishinda nchi nyingine tatu ambazo ni Romania, Georgia na Latvia na sasa  Estonia itachukua nafasi ya Poland inayomaliza muda wake.

Baraza la Usalama lina jumla ya wanachama 15 ambapo 10 wasio wa kudumu hivi sasa Ubelgiji, Cote d’Ivoire, Equatorial Guinea, Jamhuri ya Dominika, Ujerumani, Indonesia, Kuwait, Peru, Poland na Afrika ya Kusini.

Wajumbe wa kudumu ni Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Marekani.

Mgawanyo wa idadi ya uwakilishi wa wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa maeneo ni nchi 5 kutoka Afrika na Asia, 1 kutoka Ulaya, 2 kutoka Amerika ya Kusini na Karibe na 2 kutoka nchi za Ulaya Magharibi na kwingineko.