Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela sasa wafikia milioni 4:UNHCR/IOM

Wahamiaji wa Venezuela nchini Colombia. Takriban watu 5000 wamekuwa wakivuka mpaka kila siku kutoka Venezuela kwa mwaka mmoja uliopita zimesema takwimu za UN.Colombia Aprili 2019
©UNHCR/Vincent Tremeau
Wahamiaji wa Venezuela nchini Colombia. Takriban watu 5000 wamekuwa wakivuka mpaka kila siku kutoka Venezuela kwa mwaka mmoja uliopita zimesema takwimu za UN.Colombia Aprili 2019

Wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela sasa wafikia milioni 4:UNHCR/IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya raia wa Venezuela wanaofungasha virago na kuikimbia nchi yao sasa imefikia milioni 4 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR na la uhamiaji IOM. Mashirika hayo yamesema kimataifa raia wa venezuela ni moja ya kundi kubwa duniani la watu waliotawanywa kutoka nchini mwao.

Idadi ya watu wanaokimbia kutoka Venezuela imekuwa ikiongezeka kila uchao kutoka 695,000 mwishoni mwa mwaka 2015 na kufikia wakimbizi na wahamiaji milioni 4 katikati ya mwaka huu 2019 kwa mujibu wa takwimu za idara ya uhamiaji ya Venezuela na duru zingine.

IOM na UNHCR wanasema katika kipindi cha miezi saba tangu Novemba mwaka 2018 idadi ya wakimbizi na wahamiaji imeongezeka kwa milioni moja. Nchi za Amerika ya Kusini ndio wahifadhi wakumbwa wa wakimbizi na wahamiaji hao huku Colombia ikiongoza kwa kuhifadhi watu milioni 1.3, ikifuatiwa na Peru 768,000, Chile 288,000,Ecuador 263,000,Brazil 168,000 na argentina 130,000.

Mexico pamoja na nchi zingine za Amerika ya Kati na Caribbea pia zinahifadhi wakimbizi na wahamiaji kadhaa kutoka Venezuela. Katika taarifa ya pamoja ya mashirika hayo Eduardo Stein mwakilishi wa pamoja wa UNHCR na IOM kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela amesema “Idadi hii kubwa ya kutisha inaainisha haja ya kuchukua hatua haraka kuzisaidia jamii zinazowahifadhi katika nchi zinazowapokea. Nchi la Amerika ya Kusini na Caribbea zinatekeleza wajibu wao kukabiliana na mgogoro huu mkubwa, lakini hazitarajiwi kuendelea kufanya hivyo bila msaada wa kimataifa”.

Serikali katika kanda hiyo zimeanzisha mpango wa kuratibu juhudi zao na kuwezesha masuala ya kisheria, kijamii kuwajumuisha kiuchumi raia wa Venezuela. Miongoni mwa hatua hizo ni mchakato wa Quito ambao umezileta pamoja nchi za Amerika Kusini zinazokabiliwa na wimbi la wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela. Ili kukamilisha juhudi hizo mpango wa kikanda wa kuchukua hatua za kibinadamu kwa wahamiaji na wakimbizi (RMRP) ulizinduliwa Disemba mwaka jana ukiwalenga raia wa Venezuela milioni 2.2 na watu 580,000 wa jamii zinazowahifadhi katika nchi 16. Hadi sasa mpango huo wa RMRP umefadhiliwa kwa asilimia 21 pekee.