Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushrikiano na ufadhili zaidi unahitajika kwa ajili ya wakimbizi wa Venezuela-Kongamano

Mamia ya wavenezuela wakiwa mpakani mwa Colombia wakisubiri kuvuka.
UNICEF/Santiago Arcos
Mamia ya wavenezuela wakiwa mpakani mwa Colombia wakisubiri kuvuka.

Ushrikiano na ufadhili zaidi unahitajika kwa ajili ya wakimbizi wa Venezuela-Kongamano

Wahamiaji na Wakimbizi

Kongamano la kimataifa la siku mbili kuhusu janga la wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela lililoanza jana mjini Brussels Ubelgiji hadi leo 29 Oktoba 2019 limetuma ujumbe mzito kwa ajili ya msaada kwa wakimbizi na wahamiaji hao wa Venezuela pamoja na jamii zinazowahifadhi Amerika Kusini na Caribbea.

Kongamano hilo ambalo liliendeshwa na Federica Mogherini, mwakilishi wa ngazi ya juu wa masuala ya kigeni na sera za usalama wa Muungano wa Ulaya na pia makamu wa rais wa Muungano wa Ulaya, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji António Vitorino kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu janga la wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela na juhudi za nchi na jamii zinazowahifadhi.

Kongamano hilo limezingatia mafanikio ya nchi zinazowahifadhi wakimbizi, limesisitiza mshikamano wa kimataifa na juhudi za pamoja za kanda na kutoa wito kwa ushirikiano wa kimataifa na jumuishi pale mshikamano na majukumu yanabebwa na jamii nzima ya kimatifa na yanagawanywa kati ya sekta za umma na binafsi.

Zaidi ya wajumbe 120 ikiwemo taasisi za Muungano wa Ulaya na wanachama wa mataifa yaliyoathirika zaidi Amerika ya Kusini na Carribea, nchi wafadhili, mashirika ya Umoja wa mataifa, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi za kifedha za kimataifa.

Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa UNHCR, kongamano limezingatia kwa hali inayoendelea kuzorota kisiasa, haki za binadamu na janga la kijamii na kiuchumi nchini Venezuela imeibua mmoja ya hali mbaya zaidi ya ufurushwaji kushuhudiwa duniani  huku idadi ya watu wanaoondoka ikiendelea kuongezeka na raslimali na ufadhili ukishindwa kukidhi mahitaji.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi Wavenezuela milioni 4.5 wamekimbia nchi yao wengi wakielekea nchi za Amerika Kusini na Caribbea huku idadi ikitarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 6.5 kufikia mwisho wa mwaka 2020 duniani kote.

Kongamano hilo limetambua nafasi muhimu na kazi kubwa zinazozifanya nchi hizo huku pia likitambua changamoto zinazokabiliana nazo.

Washiriki wa mkutano wameonyesha dhamira yao kuendelea kulinda wakimbizi wa Venezuela na wahamiaji na kusaidi serikali za nchi zinazowahifadhi hususan katika kuhakikisha ujumuishwaji katika jamii.

Kongamano limesisitiza umuhimu wa kuunga mkono nchi zinazowahifadhi wakimbizi hao kwa kuongeza ufadhili zaidiili kuhakikisha uwasilishaji wa huduma kwa ajili ya kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wakimbizi, wahamiaji na jamii zinazowahifadhi

Kongamano limesisitiza nafasi ya jukwaa la uratibu la kikanda likiongozwa na UNHCR na IOM huku  likionyesha kukubaliana na uamuzi wa kufanya mkutano wa kwanza wa kundi la marafiki kwa ajili ya mchakato wa Quito ukiongozwa na Muungano wa Ulaya katika miezi michache ijayo.