Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Ulaya acheni kupeleka dizeli chafu na yenye sumu Afrika- Mtaalamu

Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016
© UNICEF/Bindra
Moshi wa magari, jenereta za dizeli na kuchoma taka na samadi vimesababisha uchafuzi wa hewa kwenye mij wa Lagos nchini Nigeria kama inavyoonekana kwenye picha hii ya mwaka 2016

Nchi za Ulaya acheni kupeleka dizeli chafu na yenye sumu Afrika- Mtaalamu

Haki za binadamu

Kuelekea siku ya mazingira duniani hapo kesho Juni 5 ambayo inaangazia shughuli mbalimbali za binadamu zinasochafua hali ya hewa, mtaalamu maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu taka hatarishi na za sumu ameonya kampuni za Ulaya ambazo zinauzia nchi za Afrika nishati chafuzi ikiwemo mafuta ya dizeli yenye kemikali za sumu. 

Mtaalamu huyo Baskut Tuncak amesema ni ajabu kuona kampuni hizo kutoka Ulaya zinauzia nchi za Afrika dizeli ambayo katu haiwezi kuuzwa kwenye masoko ya Ulaya, akisema tabia hiyo ikome kwa kuwa inasababisha  uchafuzi wa  hewa na vifo.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, USwisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, mtaalamu huyo amesema biashara hiyo ambayo ni kinyume na maadili na sheria akisema husababisha uchafuzi wa hewa ambayo ndio maudhui ya siku ya mazingira duniani mwaka huu.

Amesema dizeli hiyo chafu inakadiriwa kuua maelfu ya watu barani Afrika kila mwaka na idadi hiyo ya vifo inaweza kufikia 31,000 ifikapo mwaka 2030 iwapo suala hilo halitashughulikiwa.

Bi. Tuncak amesema kitendo cha kujinufaisha na viwango vidogo vilivyowekwa na Afrika ni kinyume na maadili lakini pia ni uhalifu ambao lazima uachwe na kwamba Afrika na Ulaya lazima wasake njia bora na ya wazi ya kuwa na nishati isiyo na kemikali za sumu na iliyo salama.

Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, ni uhalifu kuuzia nchi nyingine dutu zenye sumu ikiwemo nishati ambayo imepigwa marufuku kwenye nchi nyingine ambayo ni mwanachama wa Mkataba wa kimataifa wa Bamako hata kama nchi inayouza si mwanachama wa mkataba huo.

Mataifa 27 ya Afrika yameridhia mkataba wa Bamako na mtaalamu huyo ametaka serikali za Ulaya na Afrika lazima zihakikishe kuwa kampuni za biashara zinaheshimu haki za binadamu za kila mtu ikiwemo kuvuta  hewa safi.