FAO yatiwa moyo na idadi kubwa ya nchi kuridhia mkataba wa kudhibiti uvuvi haramu

4 Juni 2019

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano da Silva amekaribisha hatua ya aina yake ya mataifa zaidi ya 100 kuridhia mkataba wa kimataifa wa kuzuia uvuvi haram una usiofuata kanuni, akisema ni hatua ya kipekee.

Akizungumza mjini Santiago nchini Chile Bwana da Silva amesema mkataba huo Port State Measures Agreement au, PSMA, uliopigiwa chepuo na FAO na kuanza kutekelezwa mwaka 2016 sasa umepata nguvu kwa kuwa mataifa hayo zaidi ya 100 yameazimia kuanza kutekeleza.

"Leo hii naona chumba kilichosheheni wajumbe zaidi kuliko miaka miwili iliyopita,” amesema Bwana da Silva kwenye mkutano uliofanyika mjini Santiago kujadili jinsi ya kuchagia utekelezaji wa PSMA.

Mkataba huo unataka meli za kigeni kutia nanga katika meli za ugenini ili zikaguliwe iwapo bandari hizo zitaona ni lazima kufanyahivyo na pia nchi hizo kuwasilisha taarifa zozote za ukiukwaji wa kanuni za uvuvi.

Mkataba unaimarsha kanuni za awali ambazo ziliachia nchi yenyewe kujikagua na zaidi ya yote unaweka mfumo ambamo kwao inakuwa vigumu kwa samaki waliovuliwa kinyume cha sheria kuuzwa sokoni.

FAO inasema kiwango cha cha samaki wanaovuliwa kiharamu au kinyume na kanuni au IUU ni sawa na tani milioni 26 kila mwaka sawa na moja ya tano  ya kiwango cha samaki wote wanaovuliwa duniani kila mwaka na hivyo hudidimiza harakati za uvuvi endelevu duniani.

Akizungumzia hatua ya leo Bwana da Silva amesema "moja ya masharti muhimu ya kuwezesha PSMA kufanikiwa ni kuwa na mataifa mengi zaidi ambayo yanazuia meli za uvuvi kuvua samaki kinyume cha kanuni, la sivyo meli inaweza isitie nanga kwenye nchi husika na vivyo hivyo kwene nchi nyingine.”

Mkutano huo wa siku nne umeanza jana Jumatatu ambapo Waziri wa uchumi, maendeleo na utalii wa Chile, Jose Ramon Valente amesema umefanyika wakati muafaka kwa kuwa kuanzia sasa  hadi mwaka 2050 watu wengi zaidi duniani watahitaji protini isiyo na mafuta bandia na hiyo inapatikana kwenye mazao ya baharini.

Mkutano huo  unaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukabiliana na uvuvi haramu na usiofuata kanuni ambayo ni kesho Juni 5.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter