Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulaji wa samaki Afrika Mashariki bado uko chini- #SOFIA2018

Mfanyakazi akipakua shehena ya samaki
FAO
Mfanyakazi akipakua shehena ya samaki

Ulaji wa samaki Afrika Mashariki bado uko chini- #SOFIA2018

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Uzalishaji wa samaki duniani kwa mwaka 2016 ulikuwa tani milioni 171, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa, imesema ripoti mpya ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kuhusu hali ya uvuvi na uzalishaji wa mazao ya bahari.

Ripoti hiyo imesema asilimia 88 ya samaki hao walitumiwa kama kitoweo, ikitaja sababu ya ongezeko la kiwango hicho kuwa kutokuwepo kwa zahma kwenye uvuvi, udhibiti kwenye uvuvi na ukuaji wa ufugaji wa samaki.

FAO inasema kwa wastani mtu mmoja duniani alikula kilo 20.3 za samaki mwaka 2016 na kwamba tangu mwaka 1961 ongezeko la ulaji wa samaki limekuwa maradufu kama ilivyo ongezeko la idadi ya watu.

Kwa mantiki hiyo FAO imesema hiyo ni ushahidi dhahiri ya kwamba sekta ya uvuvi ni muhimu katika kufanikisha lengo la FAO la dunia bila njaa na utapiamlo.

Ingawa hivyo katika nchi za Afrika Magharibi mtu mmoja alikula kilo 14 za samaki kwa mwaka huo wa 2016 ilhali kwa nchi za Afrika Mashariki ni kilo 5 kwa mtu mmoja kwa mwaka.

Wavuvi wakipakua samaki aina ya jodari kwenye moja ya viwanda vya kuchakata samaki huko Abidjan, Côte d’Ivoire.
FAO/Sia Kambou
Wavuvi wakipakua samaki aina ya jodari kwenye moja ya viwanda vya kuchakata samaki huko Abidjan, Côte d’Ivoire.

FAO imesema kiwango hicho kidogo kinatokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kwa kasi kubwa kuliko uzalishaji wa samaki, sekta duni ya uzalishaji wa mazao ya bahari na ukosefu wa soko na njia za mauzo zinazofaa.
 
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema licha ya kuimarika kwa teknolojia, nchi nyingi hususan zinazoendelea bado zinakosa miundomsingi toshelezi na huduma ya kuhakikisha ubora wa samaki kwa mfano usafi, umeme na majokofu.

Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia Kanuni ya Maadili yauvuvi wa Uvuvi (CCRF)  kama muongozo katika sekta ya uvuvi na mazao ya bahari kwa ajili ya kufanikisha malengo ya  maendeleo endelevu, SDGs kupitia sekta hiyo.

Ripoti hii ikipatiwa jina la #SOFIA2018 inafuatia utafiti na mchakato wa miezi 18 ulioanza mwezi Januari mwaka 2017.