Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katu kambi za wakimbizi wa ndani hazipaswi kushambuliwa na kuporwa- UN

Mwanamke huyo na mtoto wake waliokoka chini yamkokoteni yao ni miongoni mwa maelfu ambao wamekimbia vurugu na sasa wamehifadhiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salam, Darfur Kusini (maktaba).
Photo: Albert Gonzalez Farran/UNAMID
Mwanamke huyo na mtoto wake waliokoka chini yamkokoteni yao ni miongoni mwa maelfu ambao wamekimbia vurugu na sasa wamehifadhiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salam, Darfur Kusini (maktaba).

Katu kambi za wakimbizi wa ndani hazipaswi kushambuliwa na kuporwa- UN

Amani na Usalama

Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan, Gwi-Yeop Son amelaani vikali mashambulizi dhidi ya ofisi za kibinadamu na uporaji wa mali na vifaa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kalma huko Nyala Darfur kusini.

Taarifa iliyotolewa na mratibu huyo hii leo huko Khartoum Sudan imesema shambulio hilo la juzi Jumanne ni la kulaaniwa vikali na mamlaka lazima zifanye uchunguzi haraka ili wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Tukio hili si la kwanza, kwa mujibu wa Bi. Son akisema kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, kumekuwepo na matukio kama mawili ya uporaji wa vifaa vya kibinadamu kwenye kambi za wakimbizi wa ndani jimboni Darfur.

“Inatia hofu zaidi kwa kuwa matukio haya  yanafanyika kwenye kambi za wakimbizi wa ndani ambako kunatambuliwa kuwa ni eneo la kibinadamu ambako wakimbizi wa ndani na mashirika ya misaada hayapaswi kukumbwa na vitisho, manyanyaso, mashambulizi au majeraha,” amesema Bi. Son.

Amekumbusha kuwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wanaotoa huduma za misaada ni kinyume na sheria za kibinadamu na zinaharibu mwenendo wa usambazaji misaada ya uokoaji wa maisha kwa wale wanaohitaji.

Kambi  ya wakimbizi ya ndani ya Kalma ni moja ya kambi kubwa zaidi jimboni Darfur ikiwa ni makazi ya wakimbizi wapatao 128,000.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu nchini Sudan yanalaani aina zote za ghasia na yanatoa wito kwa wadau kuheshimu, kuwezesha na kulinda operesheni za usambazaji wa misaada ya kibinadamu nchini humo.

Mwaka huu pekee wa 2019, wadau wa kibinadamu nchini Sudan wanalenga kufikisha misaada ya kibinadamu kwa watu milioni 4.4 nchini Sudan.