Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID inaendelea na operesheni zake Darfur, wakati Sudan ikishuhudia mabadiliko ya kisiasa-Mamabolo

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili maendeleo ya Sudan tarehe 17 Aprili 2019
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili maendeleo ya Sudan tarehe 17 Aprili 2019

UNAMID inaendelea na operesheni zake Darfur, wakati Sudan ikishuhudia mabadiliko ya kisiasa-Mamabolo

Amani na Usalama

Mabadiliko ya kisiasa ya mamlaka nchini Sudan yana athari za wazi kuhusu hali jimboni Darfur, amesema Mwakilishi maalum wa Ujumbe wa  pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, jimboni humo, UNAMID.

Akihutubia Baraza la Usalama katika kikao maalum kikimulika hali ya Darfur, mwakilishi huyo Jeremiah Mamabolo amesema, “tangu kuondolewa kwa Rais Omar al-Bashir , wakimbizi wa ndani na waandamanaji wengine jimbo la Darfur wameendelea kutekeleza vitendo vya kikatili."

Bwana Mamabolo ameelezea mashambulizi yaliyofanywa na chama tawala katika uwanja wa ofisi za usalama wa taifa na huduma za usalama (NISS) pamoja na katika makazi ya viongozi wa kijamii wanaodaiwa kushirikiana na mamlaka waliokuwa wakishika usukani

Matukio mengine yalifanyika katika mitaa mingi jimboni Darfur ikiwemo,  El Fasher, Nyala, Kass, Zalingei, Golo, Nertiti, Kutum, Kabkabiya, Saraf Umra, El Geneina na Mornei.

Katika kambi ya Kalma mapigano kati ya makundi ya vijana Aprili 13 yalisababisha watu 15 kuuawa.

Hata hivyo Mkuu huyo wa UNAMID amesema, “kwa ujumla inaonekana kwamba vikosi vya usalama vinaendelea kudhibiti hali.

Katika muktadha huo, mwakilishi maalum huyo amehakikishia baraza hilo kwamba UNAMID iko ngangari katika kushikilia nafasi dhabiti, hususan maeneo ya Jebel Marra ambako Umoja wa Mataifa umepeleka vikosi vya usalama.

Ameongeza kwamba, “operesheni za kila siku zinaendelea; tumeimarisha doria hususan katika na karibu na kambi za wakimbizi wa ndani na tunaendelea kushirikiana na wadau mashinani.”

Kuhusu usalama na wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mali zao, Mamabolo amesema kufikia sasa Umoja wa Mataifa haujalengwa.

Watu milioni 4.4 wako hatarini Sudan ikiwemo watu milioni 2.4 Darfur

Kuhusu hali ya kibinadamu, wajumbe wa baraza wameelezwa kuwa kwa muda mrefu kabla ya hali ya kisiasa inayoshuhudiwa kwa sasa Sudan, mahitaji ya  kibinadamu Darfur na katika maeneo mengine nchini yalikuwa yameongezeka kwa mujibu wa ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA.

Akihutubia baraza Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura, OCHA, Ursula Mueller amesema hali ya kiuchumi nchini Sudan imekuwa na athari kwa uwasilishaji wa huduma za kibinadamu huku kukishuhudiwa mfumuko wa bei ongezeko ya ei ya chakula na dawa.

Bi. Mueller amesema watu milioni 5.8 nchini Sudan, robo yao wakiwa Darfur hawana uhakika wa chakula, hii ikiwa ni watu milioni mbili zaidi ikilinganishwa na mwaka jana.

Aidha watu milioni 1.9 wanasalia kuwa wakimbizi wa ndani Sudan, idadi kubwa wakiwa Darfur.

Ameongeza kuwa, “ni muhimu kuhakikisha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu wakati msaada kwa ajili ya msaada endelevu Darfur na maeneo mengine ukiendelea kukabiliwa na changamoto.

Aidha Bi. Mueller ametoa wito kwa serikali kuchukua hatua katika kuimarisha operesheni za mashirika ya misaada ya kibinadamu.