Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN, AU na Sudan wakubaliana kuhusu mustakhbali wa UNAMID Darfur

Mnamo februari mwaka  2010, serikali ya Ethiopia ilitoa helikopta ya kivita kwa Muungano wa Afrika, , ili kusaidia vikosi vya ulinzi wa amani  kwenye ujumbe wa pamoja wa AU na UN huko Darfur UNAMID
Picha Ya Albert Gonzales Farran
Mnamo februari mwaka 2010, serikali ya Ethiopia ilitoa helikopta ya kivita kwa Muungano wa Afrika, , ili kusaidia vikosi vya ulinzi wa amani kwenye ujumbe wa pamoja wa AU na UN huko Darfur UNAMID

UN, AU na Sudan wakubaliana kuhusu mustakhbali wa UNAMID Darfur

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa, UN, Muungano wa Afrika, AU pamoja na serikali ya Sudan wamekubaliana kwa pamoja kuendelea kutekeleza makubaliano ya pamoja ya kuwezesha ujumbe wa pamoja wa wa UN na AU wa kulinda amani Darfur, UNAMID kuendelea kutekeleza majukumu yake wakati huu ambapo unajiandaa kuhitimisha shughuli zake.
 
Makubaliano hayo yamefikiwa mwishoni mwa mkutano wa utatu uliofanyika New York, Marekani siku ya Jumamosi.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho ikiwa na vipengele vitano imesema pande hizo mathalani zitafanya kazi kwa pamoja kufanikisha azimio namba 2429 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo la mwezi Mei mwaka huu linataka Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, pamoja na serikali ya Sudan zishirikiane kwa dhati kuanzia utekelezaji wa kupunguza taratibu kikosi cha UNDAMID, kusaidia kujikwamua kwa Darfur pamoja na kipindi cha mpito cha kukabidhi shughuli zote za UNAMID kwa serikali ya Sudan .

Ushirikiano baina ya wanawake ni muarobaini wa maendeleo hata kule mashinani kama inavyoonekana pichani walinda amani wanawake huko Darfur, Sudan wakielekeza wanawake mapishi ya maandazi.
UN /Muntasir Sharafdin
Ushirikiano baina ya wanawake ni muarobaini wa maendeleo hata kule mashinani kama inavyoonekana pichani walinda amani wanawake huko Darfur, Sudan wakielekeza wanawake mapishi ya maandazi.

Azimio liliongeza muda wa UNAMID  hadi tarehe 30 mwezi Juni mwaka 2019 ambapo idadi ya askari itapunguzwa hadi si chini ya  4,050 ilhali polisi wataongezwa lakini wasizidi 2,500 katika kipindi hicho.
Serikali ya Sudan Kusini ambayo imewakilishwa kwenye mazungumzo hayo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Abd Elghani Elnaim Awad Elkarim imehakikisha kutoa ushirikiano ikiwa usalama wa vifaa na watendaji wakati wa kipindi chote kilichosalia.

Katika mazungumzo hayo Umoja Mataifa uliwakilishwa na Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani Jean-Pierra Lacroix na msaidizi wake Atul Khare, ilhali Muungano wa Afrika uliwakilishwa na Smail Chergui, Kamishna wa amani na usalama wa AU.

UNAMID ilianzishwa tarehe 31 Julai mwaka 2007 kufuatia azimio  namba 1769 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusongesha amani Sudan kufuatia mzozo kati ya serikali na wapinzani kwenye jimbo la Darfur.