Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni kubwa ya chanjo yaanza dhidi ya kipindupindu yaanza Kivu Kaskazini, DRC.

Mama na mwana wapewa chanjo. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa  kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.
UNICEF/ Nangyo
Mama na mwana wapewa chanjo. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.

Kampeni kubwa ya chanjo yaanza dhidi ya kipindupindu yaanza Kivu Kaskazini, DRC.

Afya

Taarifa iliyotolewa na WHO hii leo mjini Geneva Uswisi na Goma Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, inasema zaidi ya watu 800,000 watachanjwa dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu huko Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC kufuatia uzinduzi wa kampeni kubwa ya chanjo uliofanyika leo.

Kampeni hiyo itatekelezwa na Wizara ya afya ya DRC kwa usaidizi wa WHO na washirika wake, chini ya udhamini wa muungano wa kimataifa wa chanjo, Gavi. Jumla ya watu 835,183 katika maeneo ya Binza, Goma, Kayina, Karisimibi, Kibirizi, Kirotshe na Rutshuru watachanjwa kufikia tarehe mosi ya mwezi Juni mwaka huu wa 2019.

Taarifa ya WHO inasema kuwa kampeni hii itatoa dozi ya kwanza ya chanjo kwa njia ya matone (OVC) kwa watu wa maeneo hayo kisha baadaye watarudi kutoa chanjo tena kwa njia hiyo ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa huo wa kipindupindu.

Zaidi visa 10,000 vya kipindupindu vimeripotiwa nchini humo tangu Januari mwaka huu 2019 na kusababisha zaidi ya vifo 240. Aidha visa vingine 80,000 vinavyosadikika kuwa vya surau vimesababisha zaidi ya vifo 1,400 hadi sasa katika mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa Gavi, Dkt Seth Berkley, anasema, “DRC inakabiliana na mkusanyiko wa majanga mengi. Wakati mlipuko wa Ebola unaendelea kusababisha madhara huko mashariki, surau na kipindupindu vinachukua maisha ya maelfu kote nchini. Ndiyo maana tunaingilia kati kupitia kampeni hii ya kipindupindu, kampeni ya surua inayoendelea na pia usaidizi wetu katika chanjo ya Ebola kote katika DRC nan chi za jirani. Hatuwezi kuruhusu mateso yasiyo ya msingi kuendelea.”

Naye Dkt Deo Nshimirimana wa WHO anasema, “kipindupindu kinazuilika. Kuwachanja watu wa Kivu Kaskazini ambao wako hatarini ni mchango mkubwa na utawalinda maelfu ya watu dhidi ya ugonjwa na pia kuongeza kiwango cha  kinga katika maeneo hayo.”

Pia zaidi ya watu milioni mbili tayari wamechanjwa nchinoi DRC katika maeneo 72 nchini humo ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya mlipuko wa surua. Watu wengine 400, 000 wanategemewa kuchanjwa. Baadaye mwaka huu Gavi inategemea kufadhili kampeni itakayowafaidisha watoto milioni 18 wa umri wa kuanzia miezi 6 hadi miezi 59 nchini DRC.