Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usikubali tumbaku ichukue pumzi yako- WHO

Matumizi ya tumbaku ndio chanzo kinachozuilika cha saratani duniani
WHO
Matumizi ya tumbaku ndio chanzo kinachozuilika cha saratani duniani

Usikubali tumbaku ichukue pumzi yako- WHO

Afya

Kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa duniani ya kutovuta tumbaku keshokutwa Ijumaa, shirika la afya ulimwenguni, WHO  linaangazia madhara ya matumizi ya tumbaku kwa mapafu ya binadamu ikielezwa kuwa zaidi ya asilimia 40 ya vifo vihusianavyo na utumiaji wa tumbaku vilihusiana na magonjwa kama saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa na Kifua Kikuu.

Ni kwa mantiki hiyo mwaka huu WHO inataka serikali na wadau ziongeze hatua za kulinda watu dhidi ya tumbaku maudhui ya siku hii yakiwa, Usikubali tumbaku ichukue pumzi yako.
Akifafanua kwa kina madhara ya matumizi ya tumbaku, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. TEdros Ghebreyesus amesema, “kila mwaka watu wapatao milioni 8 hufariki dunia kutokana na tumbaku. Mamilioni wengine wanaishi na magonjwa sugu kama vile saratani, Kifua Kikuu, pumu au magonjwa sugu ya njia ya hewa  yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku.”

Dkt. Ghebreyesus amesema “mapafu yenye afya ni muhimu kwa mtu kuishi maisha yenye afya. Leo na kila siku  unaweza kulinda mapafu yako na  yale ya rafiki zako na familia yako kwa kusema kukataa kutumia tumbaku.”

WHO inasema matumizi ya tumbaku hayajaacha watoto salama kwa kuwa, “zaidi ya watoto 60,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 hufariki dunia kutokana na kuvuta moshi watu wavutao sigara. Wale wanaoishi hadi kufikia utu uzima wako kwenye nafasi kubwa zaidi ya kupata magonjwa sugu ya njia ya hewa pindi wanapokuwa wakubwa.”

Ni kwa vipi moshi wa sigara unaharibu mapafu?

WHO inasema kwamba "mvuto mmoja tu wa moshi wa sigara una mamia ya kemikali za sumu ambazo huanza kuharibu mapafu. Hi ini kwa sababu pindi moshi unapovutwa, mifumo ya kusafisha makohozi na uchafu kutoka kwenye mapafu inadhoofishwa na hivyo kuruhusu sumu iliyomo kwenye tumbaku kuingia kwenye mapafu kwa urahisi."

Shirika hilo linasema kuwa matokeo yake, uwezo wa mapafu kufanya kazi unapungua na mvutaji anaanza kukosa pumzi na hivyo kusababisha njia za hewa kuanza kuvimba na kujenga makohozi, "na hivi ndivyo ambavyo tumbaku huanza kuharibu mapafu."

 

Kibao cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara kwenye eneo la bustani ya  mboga katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani.
UN News/Yasmina Guerda
Kibao cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara kwenye eneo la bustani ya mboga katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Sasa nini kifanyike?

Kuhusu nini cha kufanya, WHO inasisi serikali zitokomeze janga la tumbaku kwa kutekeleza kwa kina mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumzi ya tumbaku, FCTC na kuimarisha hatua dhidi ya matumizi ya tumbaku.

Hatua hizo ni pamoja na kupunguza matumizi ya tumbaku kwa kuongeza kodi ya bidhaa hizo, kutenga maeneo ambayo kwamo mtu haruhusiwi kuvuta sigara na kusaidia wale ambao wanataka kuondokana na uvutaji wa sigara.

Na kwa ngazi ya familia, WHO inasihi wazazi na viongozi wa kijamii kuchukua hatua kulinda afya za wanafamilia kwa kuwaeleza kinagaubaga madhara ya matumizi ya tumbaku na mbinu za kujiepusha na matumizi.

WHO inasisitiza kuwa udhibiti wa tumbaku utasaidia kufanikisha kupunguza kwa theluthi moja ifikapo mwaka 2030 idadi ya watu wanaofariki dunia kabla ya muda wao kutokana na kuvuta tumbaku na kwamba kwa hali ilivyo sasa bado dunia haiko kwenye mwelekeo wa kutimiza lengo hilo.