Hali ya Libya inazidi kututia wasiwasi- IOM na UNHCR

14 Mei 2019

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kushughulikia wahamiaji IOM na la kuhudumia wakimbizi UNHCR, hii leo mjini Geneva Uswisi yamesema yanaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa na hali inayoendelea nchini Libya.

Kwa mujibu wa takwimu za  wakimbizi wa ndani zilizotolewa na IOM, hivi sasa kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani 66,000, takribani familia 13,310 kutoka katika maeneo yaliyoathirika mjini Tripoli nchini Libya, tangu kuanza upya kwa mgogoro tarehe 4 mwezi Aprili mwaka huu.

IOM imesema hali ni ya kutisha hasa kwa zaidi ya wahamiaji 3,300, kati yao wakiwa watoto na wanawake wajawazito.

Aidha IOM imesema ina wasiwasi juu ya wahamiaji wanaorejea katika bandari isiyo salama na pia kwa namna wanavyohifadhiwa katika vituo ambavyo vimefurika watu wengi ambako hali haikubaliki.

Mkuu wa IOM nchini Libya, Othman Belbeisi amesema, “wakati watu wetu wakiendelea kutoa msaada wa dharura wa kibinadamu kwa watu walioathiriwa na vurugu, tunatambua kuwa mambo zaidi yanatakiwa kufanyika kutoka pande zote ili kuhakikisha usalama wa wananchi. Tuna wasiwasi kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu mjini Tripoli na tunarudia kusema kuwa kuna umuhimu mkubwa kusitisha kuwashikilia wahamiaji katika vituo na pia kusitisha watu kupoteza makazi.”

Kwa upande wa UNHCR, msemaji wake Charlie Yaxley amesema wanaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama mjini Tripoli kutokana na kuwepo kwa mapigano na  mashambulizi ya anga mjini kote.

Bwana Yaxley amesema katika siku chache za hivi karibuni kumekuwa mashambulizi ya anga na makombora yamekuwa yakirushwa katika maeneo ya Ain Zara, Tajoura pia karibu na uwanja wa kimataifa wan de wa Tripoli.

“Maelfu ya raia, wamekuwa wakihama kila siku kuelekea katika maeneo salama ya mji na pia kuelekea katika milima ya Nafusa. Mahijati ya kibinadamu yanaongezeka huku chakula na dawa vikiwa haba na kukiwa na ugumu wa kutembea katika mji. UNHCR inaendelea kufuatilia mahitaji ya wahamiaji, kusambaza blanketi, magodoro na vifaa vingine muhimu," amesema Charlie Yaxley.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter