Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Chonde chonde tuvumiliane, tushikamane na kuzima moto wa hotuba za chuki:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiweka shada la m aua huko Christchurch New Zealand kuenzi waathirika wa shambulio la Machi mwaka huu.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiweka shada la m aua huko Christchurch New Zealand kuenzi waathirika wa shambulio la Machi mwaka huu.

 Chonde chonde tuvumiliane, tushikamane na kuzima moto wa hotuba za chuki:Guterres

Amani na Usalama

Katika siku ya tatu ya ziara yake nchini New Zealand , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa heshima zake kwa waathirika wa shambulio la kikatili kwenye misikiti mjini Christchurch ambako waislam zaidi ya 50 walipigwa risasi na kuuawa katika matukio mawili tofauti Ijumaa ya Machi 15 mwaka huu.

Guterres ametoa wito wa mshikamano kupambana na hotuba za chuki zilizoshika kasi hivi karibuni alipozuru misikiti yote miwili iliyoathirika, Linwood ambako ameweka shada la maua na Al Noor.

Machi 15 mwaka huu mtu mwenye silaha aliuwa watu 51 katika misikiti miwili huku akirekodi moja kwa moja ukatili huo wa shambulio lake kwenye mitandao ya kijamii. Akiwa kwenye msikiti wa al Noor mapema leo Guterres ameiambia jamii ya Kiislam ya eneo hilo kwamba, “najua hakuna maneno ambayo yanaweza kuwaondolea maumivu, huzuni na machungu , lakini nilitaka kuja hapa binafsi ili kuwafikishia upendo, msaada na kuwashika mkono. Jamii hii inadhihirisha mshikamano ambao imeufahamu kwa muda ambao uko ndani ya Uislam, ambao ni imani ya upendo, huruma , msamaha na huruma.”

Alikumbusha kwamba wakati akiwa kamishina mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa alishuhudia ukarimu w anchi za Kiislam zikifungua mipaka yake kwa watu waliokuwa wakikabiliwa na madhila kutoka sehemu mbalimbali duniani ambako sehemu nyingine nyingi mipaka yao ilifungwa.

Katibu Mkuu pia amesema kwa wakati kama huu ulioghubikwa na madhila kila kona ya dunia umoja unakuwa ni nguvu kubwa akisema, “ni lazima tushikamane katika kipindi hiki kigumu. Hotuba za  chuki zinaenea na mtazamowa umma umebadilishwa. Mitandao ya kijamii inatumiwa kama jukwaa la kusambaza chuki. Lazima tuonyeshe ushirikiano katika kukabiliana na hatari hii kubwa ya chuki. "

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipotembelea jamii wa waislamu huko Christchurch nchini New Zealand
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipotembelea jamii wa waislamu huko Christchurch nchini New Zealand

Hakuna fursa ya hotuba za chuki

Katibu Mkuu ameainisha mikakati miwili ambayo itasaidia kulinda maeneo ya ibada na kupambana na hotuba za chuki. Amemuomba mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya muungano wa ustaarabu Miguel Moratinos, kuandaa mpango wa hatua kwa ajili ya Umoja wa Mataifa ili kushiriki kikamilifu kusaidia kulinda maeneo ya kidini.

Pia amemuomba mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng, ili kuleta pamoja timu ya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia hotuba za chuki na kuwasilisha mkakati wa kimataifa wa hatua hizo. Amesisitiza kuwa “hotuba za chuki zinasambaa kama moto wa nyikani , ni lazima tuuzime, hakuna nafasi kwa hotuba za chuki kwenye mitandao na nje ya mitandao.”

Guterres ameishukuru jumuiya ya waislam wa Christchurch kwa kusaidia dunia kuwafahamu na kufahamu utu, akisisitiza kwamba katika wakati huu wa majaribu yuko hapo kuwahakikishia kwamba hawako peke yao, dunia nzima iko pamoja nao naye yuko pamoja nao.

Ziara hii ya Katibu Mkuu New Zealand ni sehemu ya ziara yake katika mataifa ya Pasifiki ili kuchagiza masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Kesho jumatano atahutubia jukwaa la visiwa vya Pasifiki ambalo mwaka huu linafanyika Fiji kabla ya kuelekea Tuvalu na Vanuatu.