Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wa rangi unakita mizizi na hauna nafasi katika karne hii:UN

Watoto wa mjini Cape Town Afrika Kusini miaka ya 1980 nyakati ambazo weusi na weupe hawakuruhusiwa kuoana.
UN
Watoto wa mjini Cape Town Afrika Kusini miaka ya 1980 nyakati ambazo weusi na weupe hawakuruhusiwa kuoana.

Ubaguzi wa rangi unakita mizizi na hauna nafasi katika karne hii:UN

Masuala ya UM

Umefika wakati wa kusema sasa imetosha, ubaguzi wa rangi , chuki dhidi ya wageni na mifumo mingine yoyote ya chuki na ubaguzi haina nafasi katika karne hii, amesema Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet. 

Katika ujumbe wake maalumu kuhusu siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi iliyobeba  kaulimbiu “ kupunguza na kukabiliana na ongezeko la itikadi na misimamo mikali ya kibaguzi” Bi. Bachelet amesema lengo ni kuhakikisha hatua zinachukuliwa kudhibiti hali hiyo ambayo inachagiza ajenda za kitaifa zenye ubaguzi zinasambaa sehemu mbalimbali duniani, na kuchochea ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni, na hali zingine za kutovumiliana ambazo mara nyingi zinawalenga wahamiaji na wakimbizi lakini pia watu wenye asili ya Afrika. Akisistiza kwamba,“Utaifa na ubaguzi wa rangi havitoi suluhu yoyote ya changamoto zinazozikabili jamii hivi sasa , vinatokana na misingi ya nadharia na kuzagazwa na kukuzwa na mitandao ya kijamii . Na hatua hii imepanda mbegu za hasira na kuvuna chuki na machafuko, suala hili la utaifa ni kinyume kabisa na uzalendo, kwani linaongeza mgawanyiko, linaandaa ghasia na kuzifanya jamii kutokuwa salama.”

Amehimiza kuwa wote tunapaswa kukemea waziwazi ujumbe hususani wa kisiasa unaochagiza hali hiyo kwani unaweza kuipenda nchi yako lakini pia ukaipenda dunia, na unaweza kuheshimu taifa lako wakati pia ukiheshimu tofauti zilizopo na watu wengine.

Naye mtaalam huru kuhusu mifumo ya kisasa ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na kutovumiliana , E.Tenday Achiume akisistiza hilo amelaani vikali ajenda za kitaifa zinazoongeza vitendo na sera za ukandamizaji, ubaguzi na kuwatenga watu ambazo zinaathiri watu binafsi na makundi ya watu kwa misingi ya rangi zao, ukabila, nchi watokako na dini zao. Akitolea mfano shambulio la wiki iliyopita Christchurch nchini New Zealand na kukatili maisha ya watu 50.

Amezitaka nchi kusimama kidete kuchukua hatua kukomesha hali hiyo kama haijageuka na kuwa ada.