Watu zaidi ya 40 wauawa kikatili msikitini New Zealand, UN yalaani.

15 Machi 2019

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio kwenye misikiti miwili nchini New Zealand lililokatili na kujeruhi watu wengi leo mjini Christchurch. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia ukurasa wake wa twitter ameandika "nimeshtushwa na ninalaani vikali kitendo cha kuwapiga risasi watu wasio na hatia wakiswali kwa amani misikitini New Zealand. Natoa rambirambi zangu za dhati kwa familia za waathirika . Leo na kila siku ni lazima tushikamane kupinga chuki dhidi ya Waislaam na mifumo yote ya kibaguzi na ugaidi."

 

Kwa mujibu wa duru za habari watu zaidi ya 40 wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine 20 kujeruhiwa katika misikiti miwili eneo la Christchurch nchini New Zealand. Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa pia yanaelezea hisia zao kufuatia tukio hilo akiwemo mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika “nimeshitushwa sana na kupotea kikatili kwa maisha ya watu kufuatia mashambulizi mawili kwenye misikiti nchini New Zealand , misikiti ambayo ilikuwa imefurika waumini wakihudhuria swala ya Ijumaa. Inaaminika kwamba miongoni mwa waliokufa na kujeruhiwa wengi ni wakimbizi na wahamiaji . Napenda kutuma salamu zangu za rambirambi kwa familia za waathirika wote na serikali na watu wote wa New Zealand.”

 

Naye kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR , Filippo Grand ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema “Sote hapa katika shirika la wakimbizi la UNHCR tunasimama pamoja na wat una serikali ya New Zealand  kuomboleza, kusali na kushikamana na nanyi.”

 

Waziri mkuu wa nchi hiyo Jacinda Arden akiita mashambulizi hayo ni kitendo cha kigaidi na leo ni moja ya siku za giza totoro nchini humo.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter