Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo vya Marekani vinakiuka haki za binadamu na kanuni za kimataifa za maadili-Mtaalam

Idriss Jazairy, Mtaalamu Maalum wa UN kuhusu madhara ya vikwazo  vinavyoathiri haki za binadamu
UN/Eskinder Debebe
Idriss Jazairy, Mtaalamu Maalum wa UN kuhusu madhara ya vikwazo vinavyoathiri haki za binadamu

Vikwazo vya Marekani vinakiuka haki za binadamu na kanuni za kimataifa za maadili-Mtaalam

Haki za binadamu

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa Idriss Jazairy ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua za hivi karibuni za Marekani dhidi ya Cuba, Venezuela na Iran akisema matumizi ya vikwazo vya kiuchumi kwa madhumuni  ya kisiasa inakiuka haki za binadamu na kanuni za tabia ya kimataifa.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Bwana Jazairy amesema hali hiyo inaweza kusabahisha majanga ya kibinadamu makubwa yanayosababishwa na binadamu, mtaalamu huyo ameeleza.

Bwana Jazairy amesema, “mabadiliko ya utawala kupitia hatua za kiuchumi ambazo zina uwezekano wa kusababisha kukiuka kwa haki za binadamu na uwezekanao wa kusababisha baa la njaa havijawahi kukubalika katika mahusiano ya kimataifa. Masuala ya msingi na tofauti za kisiasa kati ya serikali mbalimbali havipaswi kuamriwa kamwe kwa kuingiza vikwazo vya kiuchumi na hatimaye kuwafanya watu wa kawaida kuwa mateka.”

Aidha mtaalamu huyo amefafanua kuwa, utekelezaji wa Hati ya III wa sheria za vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba ambayo inawaruhusu wananchi wa Marekani kufungua kesi dhidi ya kampuni za Cuba na kampuni ya kigeni kuhusiana na mali zilizokamatwa na kutumika baada ya mapindsuzi yam waka 1959 ya Fidel Castro, ni kupuuza mapingamizi yaliyofanywa na Muungano wa Ulaya na Canada n ani mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya makampuni ya Ulaya na Canada nchini Cuba ambako wao ndiyo wawekezaji wakubwa wa kigeni.

Mnamo tarehe 17 mwezi Aprili mwaka huu, Marekani ilipiga marufuku Benki kuu ya Venezuela kufanya miamala yoyote ya dola ya kimarekani baada ya tarehe 17 mwezi huu wa Mei na watafunga kupata huduma za kibinadamu nchini Marekani ifikapo mwezi Machi 2020.

“Ni vigumu kufahamu ni kwa namna gani hatua ambazo zina matokeo ya kuharibu uchumi wa Venezuela na kuwazuia wavenezuela kutuma fedha nyumbani, kunavyoweza kulenga kuwasaidia watu wa Venezuela kama Marekani inavyodai.” Amehoji mtaalamu huyo.

Tamko lake hili limekuja baada ya ripoti za hivi karibuni kudai kuwa watu 40,000 wamepoteza maisha nchini Venezuela tangu mwaka 2017 kwasababu ya vikwazo vya Marekani.