Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikwazo mnavyowekeana visiguse raia- Mtaalam

Idriss Jazairy, Mtaalamu Maalum wa UN kuhusu madhara ya vikwazo  vinavyoathiri haki za binadamu
UN/Eskinder Debebe
Idriss Jazairy, Mtaalamu Maalum wa UN kuhusu madhara ya vikwazo vinavyoathiri haki za binadamu

Vikwazo mnavyowekeana visiguse raia- Mtaalam

Haki za binadamu

Msemo wa wahenga kuwa wapiganapo mafahali wawili ziumiazo ni nyasi unadhihirika nchini Iran ambako imeelezwa kuwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo kama shinikizo la kisiasa, vimekuwa ‘mwiba’ kwa raia.
 

Hiyo ni kwa mujibu wa mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa ambaye amesema vikwazo vya kiuchumi ambavyo vinavuka mipaka ya nchi na kulenga kuzuia nchi nyingine kibiashara ni sawa na vita vya kiuchumi dhidi ya raia.
Mtaalamu huyo Idriss Jazairy anayehusika na madhara ya vikwazo vya kiuchumi kwa haki za binadamu, amesema hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Amesema “hawa raia wana haki ya kulindwa na mkataba wa Geneva kuhusu watu vitani. Kuna umuhimu wa tofauti kati ya mataifa kutatuliwa kwa njia za amani huku raia wasio na hatia wakilindwa dhidi ya adhabu ya jumla kama ilivyobainishwa na katiba  ya Umoja wa Mataifa.”
Bwana Jazairy amesema kutumbukizwa raia kwenye adhabu hiyo ya jumla husababisha njaa na magonjwa na kwamba mbinu hizi za vikwazo vya kiuchumi hazipaswi kukubaliwa kwenye karne hii ya 21.
Ametolea mfano wa Iran ambayo licha ya vikwazo vya Marekani kutojumuisha mahitaji ya kibinadamu, kuna ripoti ya kwamba misaadda inashikiliwa kwenye benki kwa kuwa kampuni zinasubiri ufafanuzi kuhusu kipi kinahusika na vikwazo na kipi hakihusiki.
“imeelezwa kuwa nchi ambayo imewekea Iran vikwazo itazuia mfumo wa kuhamisha fedha na hivyo kukwamisha miamala ya fedha baina ya benki,” amesema Bwana Jazairy.
Ameongeza kuwa “hakuna lolote la kuhalalisha hali hii ikiwemo vikwazo vya jumla kwenye uagizaji chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu ambapo taratibu za kuingiza nchini humo ni ndefu na zina vikwazo.”
Mtaalamu huyo amesema kinachomsikitisha zaidi ni kwamba raia maskini ndio wanabeba mzigo wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, watu wakipoteza kazi, uchumi unadumaa na thamani ya sarafu ya Iran inazidi kudidimia.
Amesema ingawa haki ya nchi kutokubaliana na nchi nyingine inapaswa kuheshimiwa, “kuumiza raia wa kawaida hakupaswi kuwa ndio jaribio la mwisho la kufanikisha shinikizo la kisiasa kwa serikali. Hii ni kinyume kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa.”
Bwana Jazairy amesema yuko tayari kuwa mwezeshaji wa kusaidia Marekani na Iran kusaka njia bora zaidi kuhakikisha vikwazo hivyo havigusi misaada ya kibinadamu.
Marekani ilirejesha tena vikwazo vyake dhidi ya Iran hivi karibuni.