Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatoa mwongozo kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijitali kuwasilisha huduma za afya

Teknolojia ya simu za kiganjani imefungua milango ya biashara kwa wengi wanaomiliki simu hizo na pia walio na fursa za mtandao wa intaneti
UN News/Nam Cho
Teknolojia ya simu za kiganjani imefungua milango ya biashara kwa wengi wanaomiliki simu hizo na pia walio na fursa za mtandao wa intaneti

WHO yatoa mwongozo kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijitali kuwasilisha huduma za afya

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa mwongozo wa vipengele 10 ambavyo nchi zinaweza kutumia kwa ajili ya teknolojia ya kidijitali ili kuimarisha huduma ya afya ya binadamu kupitia simu za mkononi na kompyuta. Arnold Kayanda na maelezo zaidi.

Taarifa ya WHO imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus  akisema, “matumizi ya teknolojia ya kidijitali ni muhimu kwa ajili ya kufikia uwasilishaji wa huduma ya afya kote ulimwenguni.

Ameongeza kuwa “sio kwamba teknolojia za kidijitali ndio hatma; lakini ni vifaa muhimu katika kuimarisha afya, kuweka ulimwengu salama na kuhudumia walio hatarini.”

WHO ilitathmini teknolojia za kidijitali na kushauriana na wataalam na kufikia mapendekezo hayo, na tayari kuna matokeo chanya katika baadhi ya maeneo kwa mfano kutuma ujumbe kwa wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki na kurudisha watoto hospitalini ili wapate chanjo.

Matumizi mengine ya teknolojia hiyo ni kama vifaa vya kutoa muongozo kwa watoa huduma na kuwezesha watu binafsi na wahudumu wa afya kuwasiliana na kushauriana kuhusu maswala ya kiafya katika maeneo tofauti.

 Dkt. Soumya Swaminathan, ni mwanasayansi mkuu katika WHO ambaye amesema “matumizi ya teknolojia ya kidijitali inatoa fursa mpya za kuimarisha afya ya watu lakini ushahidi unaonesha changamoto katika matokeo ya baadhi ya huduma, iwapo teknolojia za kidijitali zitakuwa endelevu na kuingizwa katika mfumo wa afya, ni lazima zichangie katika kuimarisha mbinu za kijadi za kuwasilisha huduma za afya.”

WHO imesisitiza kwamba mbinu za kidijitali zinategemea kwa kiasi kikubwa mfumo na utaratibu fulani na ikiwemo muundo na miundombinu iliyopo na mahitaji ya kiafya ambayo inakusudia kukabiliana nayo.

Mifumo ya kidijitali pekee haitoshi 

Mapendekezo yanaonesha kwamba mifumo ya kiafya inahitaji kuitikia ongezeko la taarifa na uwepo wake na kwamba watu wanahitaji kuhakikishiwa kwamba taarifa zao ziko salama na kwamba hawatawekwa hatarini kwa sababu wamesoma taarifa kuhusu mada kama vile masuala ya kingono au masuala ya afya ya uzazi.

Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.
UNICEF/Christine Nesbitt
Mama na mwanae mchanga wakipata huduma baada ya kujifungua kwenye wodi ya wazazi iliyoko kliniki ya Shakawe nchini Botswana.

Kwa upande wa wahudumu wa afya, WHO imesema mafunzo toshelezi yanahitajika kwa ajili ya kuweza kutumia teknolojia hiyo kwa urahisi. Aidha mapendekezo yanahimiza umuhimu wa kuweka mazingira yanayowezesha kwa ajili ya kutoa mafunzo na kukabiliana na miundo mbinu inayosuasua na sera kwa ajili ya kulinda faragha ya watu binafsi na usimamizi na ufuatiliaji kuhakikisha vifaa hivyo havitawanyiki katika mfumo wa afya.

Mwongozo huo wa WHO unatoa mapendekezo kuhusu dawa kupitia teknolojia ambayo inawezesha watu wanaoishi mashinani kupata huduma za afya kupitia simu za mkononi, au vifaa vingine vya kdijitali.

Hata hivyo WHO imesema hatua hii inaendana vizuri na mawasiliano ya ana kwa ana lakini haiwezi kuchukua nafasi hiyo kwa ujumla.

Aidha WHO imeongeza ni muhimu kwamba mashauriano yatolewe na wahudumu wa afya na kwamba faragha ya taarifa za kiafya za watu binafsi izingatiwe.

Mwongozo unasisitiza umuhimu wa kufikia watu walio hatarini na kuhakikisha kwamba afya ya kidijitali haiwaathiri kwa vyovyote vile.