Labda awe amelala lakini sasa mfanyakazi afanya kazi zaidi ya saa 48 kwa wiki-ILO

Wafanyakazi kutoka Syria wakichambua tumbaku kwenye kiwanda kimoja nchini Lebanon (Maktaba)
ILO/Deloche P
Wafanyakazi kutoka Syria wakichambua tumbaku kwenye kiwanda kimoja nchini Lebanon (Maktaba)

Labda awe amelala lakini sasa mfanyakazi afanya kazi zaidi ya saa 48 kwa wiki-ILO

Afya

Ripoti mpya ya shirika la kazi duniani ILO inasema kila siku watu 7500 hufariki dunia kutokana na mazignira yasiyo salama na afya kazini. 

Mabadiliko ya mazingira ya kazi, teknolojia za kisasa na kitendo cha mtu kuweza kufanya kazi popote pale alipo na wakati wowote pamoja na ukosefu wa usalama kazini ni sehemu tu ya mambo yanayosababisha vifo hivyo kila uchao kote duniani.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina usalama na afya kama kitovu cha mustakabali wa  kazi, kujenga kutokana na uzoefu wa miaka 100 ya ILO, inasema kando ya idadi hiyo, kila mwaka watu zaidi ya milioni 374 wanajeruhiwa au wanaugua kutokana na ajali kazini ikiwemo kufanya kazi muda mrefu.

Manal Azzi, ni mtaalamu wa ILO kuhusu usalama kazini anasema labda uwe umelala lakini kila wakati mfanyakazi anaweza kufikiwa na kutakiwa kufanya kazi.

“Watu mbalimbali wanafanya kazi kwa njia mbalimbali ikiwemo simu, kompyuta mpakato unazoweza kwenda nazo kila pahali. Intaneti inapatikana kwa kila mtu, simu za kimataifa zinafanya mtu aweze kupatikana wakati wowote.”

Manal anasema katika mazingira hayo wafanyakazi wanatakiwa kufanya  kazi zaidi na zaidi na hawana muda wa kupumzika hali inayoweza kusababisha magonjwa ya akili, msongo wa mawazo na hata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani na moyo.

Mshiriki katika tamasha la Marekani la sayansi na uhandisi (2014) akiangalia jukwaani roboti wa kwanza mithili ya binadamu ajulikanaye kama Robonaut 2. wakati huo Roboti huyo (R2) alikuwa ndio kwanza amewekewa miguu mirefu ya kumruhusu kutembea.
NASA/Aubrey Gemignani
Mshiriki katika tamasha la Marekani la sayansi na uhandisi (2014) akiangalia jukwaani roboti wa kwanza mithili ya binadamu ajulikanaye kama Robonaut 2. wakati huo Roboti huyo (R2) alikuwa ndio kwanza amewekewa miguu mirefu ya kumruhusu kutembea.

 

Vichochezi vya mazingira hatarini ya pahala pa kazi

ILO inataja mambo manne ambayo pamoja na kuchochea mazingira hatarishi ya sasa yanaweza kutumiwa vyema ili kuboresha mazingira ya pahala pa kazi siku za usoni.

Mosi:

Teknolojia kama vile matumizi ya mifumo ya kidijitali, maroboti ambazo zinaweza kuathiri afya ya kisaikolojia ya mfanyakazi na kwa kuwa zinatumia dutu za kisasa athari zake za kiafya bado hazijapimwa na kutathmini vya kutosha. Iwapo zitatumia vyema zinaweza kupunguza hatari kazini, kufanikisha mafunzo na pia kaguzi sehemu za kazi.

Pili:

Mabadiliko ya umri na jinsi ya wafanyakazi ambapo wanawake wanaoajiriwa wanaongezeka lakini bila kuzingatia viwango bora vya mazingira ya kazi na hivyo hatarini kupata magonjwa ya misuli na mifupa.

Tatu:

Maendeleo na mabadiliko ya tabianchi vinatumbukiza wafanyakazi kwenye hewa chafuzi, shinikizo la joto na hata wengine kupoteza kazi. Fursa mpya za ajira zinaweza kupatikana kupitia mikakati ya maendeleo endelevu na kazi zisizoharibu mazingira..

Nne:

Mabadiliko ya utendaji wa kazi yanaruhusu watu wengi kuajiriwa na wakati huo huo wanafanya kazi zinazowaletea shinikizo na pia hofu ya kupoteza kazi na kuingiliwa kwa faragha yao. Mathalani kufanya kazi bila kupumzika yaani zaidi ya saa 48 kwa wiki.

ILO inapendekeza mambo sita ikiwemo será bunifu za za ajira zinazojali afya ya umma na kuimarisha sheria za viwango vya kazi kimataifa na kitaifa.

Ripoti hii imetolewa kuelekea siku ya usalama kazini duniani tarehe 28 mwezi Aprili.